Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa David Ernest Silinde ametoa miezi sita kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kukamilisha sehemu ya chini ya jengo la ofisi za Halmashauri na kuhamia katika ofisi hizo wakati ujenzi unaendelea ghorofani.
Mheshimiwa Silinde ametoa agizo hilo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri hiyo inayojengwa kwa mfumo wa force account na SUMA JKT baada ya Naibu Waziri kupokea malalamiko kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mheshimiwa Mwita Waitara.
“Ninaelekeza Halmashauri itafute vifaa ili SUMA JKT waendelee na kazi katika mradi huu na kipaumbele kwa sasa kiwe kukamilisha sehemu ya chini ya jengo hili ili liweze kuanza kutumika wakati ujenzi sehemu ya juu ukiwa unaendelea” alisema Mheshimiwa Silinde.
Amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwasilisha taarifa ya hatua za ujenzi baada ya miezi sita ili aweze kuja kukagua na kujiridhisha kama Halmashauri hiyo imeshahamia katika jengo hilo.
Mheshimiwa Silinde pia ameitaka Halmashauri hiyo kununua vifaa vyote vinavyohitajika kukamilisha jengo hili ili mradi huo usiendelee kukwama tena kutokana na kukosekana kwa vifaa vya ujenzi.
Mheshimiwa Silinde ambaye ni mbunge wa Mji wa Tunduma ameeleza kuwa katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, jengo la Halmashauri lilianza kutumika sehemu ya chini wakati ujenzi ukiendelea sehemu za juu za jengo hilo.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa hajaridhishwa na usimamizi wa jengo hilo na kusababisha mradi kuwa na maneno maneno mengi sana yasiyo na msingi wowote.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini Mheshimiwa Mwita Waitara ameeleza kuwa madiwani na watumishi wanapata shida sana kutokana na kukosekana ofisi za uhakika za kufanyia shughuli zao na hivyo kulazimika kutumia majengo mengine kwa shughuli za halmashauri.
“Vikao vya Baraza la Madiwani vinafanyika katika ukumbi au vyumba vya madarasa ya Shule ya Sekondari ya Mwalimu Julius K. Nyerere jambo ambalo linaweza kuwa linaingilia masomo ya wanafunzi” alisema Mheshimiwa Waitara.
Mheshimiwa Waitara ameeleza kuwa kinachowashangaza wananchi ni kuona ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri unaenda vizuri wakati ujenzi wa jengo la ofisi hizo hauendi vizuri.
Akizungumza katika eneo la mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Bwana Solomon Shati ameeleza kuwa mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 2.9 na mpaka sasa Halmashauri imepokea shilingi bilioni 2, na tayari bilioni 1 imeshatumika.
Bwana Shati ameeleza kuwa kwa sasa wanashindwa kununua vifaa kutokana na changamoto za mfumo wa malipo zilizojitokeza kwa nchi nzima na kuongeza kuwa vifaa vitanunuliwa mara baada ya mfumo kutengamaa.
Aidha, ameeleza kuwa mradi huo awali ulichelewa kutokana na uzembe wa SUMA JKT lakini kwa sasa hauendelei kwa sababu hamna vifaa kutokana na changamoto za mfumo wa malipo ya serikali zinazoendelea.
Bwana Shati amemhakikishia Naibu Waziri kuwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo vitanunuliwa mara baada ya mfumo wa malipo wa serikali kukaa sawa na kuiwezesha SUMA JKT kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Ujenzi wa jengo la gorofa moja la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime umeanza kujengwa mwaka 2020 na mpaka sasa bado ujenzi unaendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa