Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI), Dkt. Ntuli Kapologwe leo amefanya kikao cha majumuisho na wasimamizi wa sekta ya afya na wadau wa afya wa Mkoa wa Mara na kuwataka Waganga Wakuu wa Halmashauri kufunga mfumo wa ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya (GoTHOMIS).
Akizungumza katika kikao hicho baada ya ziara aliyoifanya katika Mkoa wa Mara, Dkt. Kapologwe ameipongeza Manispaa ya Musoma kwa kuboresha makusanyo katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka shilingi 37,210,000 mwaka 2017/2018 hadi 396,410,000 mwaka 2021/2022.
“Haya mafanikio yamekuja baada ya Manispaa ya Musoma kufunga mfumo wa kukusanyia mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya (GOTHOMIS) katika vituo vyake na kuboresha makusanyo” alisema Dkt. Kapologwe.
Aidha, amekipongeza Kituo cha Afya cha Natta katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuongeza mara dufu ukusanyaji wa mapato baada ya kufunga GoTHOMIS akilinganisha na hospitali ya Wilaya ya Serengeti ambayo haijafunga mfumo huo na kukusanya mapato kidogo huku ikiwa na watu wengi zaidi wanaopatiwa huduma.
Aidha, ameupongeza Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya katika sekta ya afya hususan katika utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 ambapo kwa sasa Mkoa wa Mara umeshika nafasi ya 9 kitaifa katika utoaji wa chanjo hiyo.
Dkt. Kapologwe amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri kushughulikia mapungufu yote yaliyoonekana wakati wa ziara hiyo na kuhakikisha kuwa mapungufu kama hayo yanatatuliwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya wa Mkoa wa Mara Dkt. Juma Mfanga ameishukuru timu ya wataalamu kutoka TAMISEMI kwa ziara na maelekezo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo hayo.
“Tunaahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na tutawasilisha taarifa ya utekelezaji wa maelekezo hayo” alisema Dkt. Mfanga.
Wakati huo huo, Dkt. Mfanga ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara ameishukuru AMREF kwa kuleta wataalamu wa afya 385 wa kada mbalimbali ili kusaidia kuboresha huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Aidha, Dkt. Mfanga amewashukuru wasimamizi wa sekta ya afya kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kwa kuitikia wito wa kikao hicho na kufika kwa wingi na kuwataka kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kwa haraka.
Katika ziara hiyo, timu ya wataalamu imefanya ziara ya siku tatu na kutembelea vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa