Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amefanya ziara ya kukagua ukarabati wa Hospitali ya Manispaa ya Musoma na kupongeza uanzishwaji wa wodi za wagonjwa wa VIP katika hospitali hiyo.
Dkt. Mfaume ametoa pongezi hizo baada ya kukagua wodi hizo na kuitaka Manispaa ya Musoma kufunga televisheni katika wodi hizo na kuboresha huduma kwa wagonjwa watakaolazwa katika wodi hizo ili kuwavutia wengi zaidi kukaa kwenye wodi hizo na kuongeza mapato ya hospitali.
“Ubunifu huu ni jambo la kuigwa na Hospitali zote za Halmashauri hapa nchini ili katika ngazi ya msingi pawepo na huduma nzuri kwa viongozi na watu wenye uwezo wa kulipia ili kuongeza mapato ya hospitali na kutoa huduma bora kwa wananchi” amesema Dkt. Mfaume.
Dkt. Mfaume ameitaka Manispaa ya Musoma ukarabati utakapokuwa umekamilika kuitangaza huduma zitakazokuwa zinatolewa hapo ikiwa ni pamoja na kuonyesha vyumba hivyo pamoja na gharama zake ili wananchi waweze kutambua mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika hospitali hiyo.
Aidha, Dkt. Mfaume amepongeza ukarabati mkubwa pamoja na ujenzi wa fensi uliofanyika katika hospitali hiyo baada ya Manispaa ya Musoma kukabidhiwa majengo ya iliyokuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara mwezi Julai, 2023 baada ya hospitali hiyo kuhamia katika majengo jengo lao lililopo eneo la Kwangwa, Manispaa ya Musoma.
Dkt. Mfaume akiwa katika eneo hilo pia, alikagua ujenzi wa majengo mapya ya wagonjwa wa dharura, kinywa na meno na macho katika hospitali hiyo ambayo ujenzi wake uko katika hatua ya boma na kuitaka Manispaa ya Musoma kuongeza kasi ya ujenzi ili wananchi waweze kupata huduma mapema.
Hata hivyo, Dkt. Mfaume ameitaka Manispaa ya Musoma kuweka mchanganuo wa ukarabati kuonyesha kila jengo limetumia shilingi ngapi na kukarabati vitanda na samani nyingine ili ziweze kutumika kutoa huduma.
Aidha, ameipongeza Manispaa ya Musoma kwa kutoa mafunzo na matumizi ya mfumo wa GoTHOMIS ulioboreshwa kwa watumishi wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika Manispaa hiyo na kuitaka Manispaa kufuatilia kibali cha kubadili matumizi ya sehemu ya fedha za ukarabati ili kujenga duka la dawa la hospitali.
Akitoa taarifa ya ukarabati huo, Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Manispaa ya Musoma Dkt. Mustafa Waziri amesema Manispaa ilipokea jumla ya shilingi bilioni 1.3 ambapo milioni 500 zilikuwa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa fensi na milioni 800 zilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya.
Dkt. Mustafa ameeleza kuwa hadi sasa ukarabati na ujenzi wa fensi umekamilika na fedha iliyobakia katika mradi huo imetumika kujenga duka la dawa la hospitali hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 39 huku ujenzi wa majengo mapya unaendelea.
Dkt. Mustafa ameeleza kuwa baada ya ukarabati, hospitali hiyo kwa sasa ina vyumba vya VIP vya gharama ya shilingi 40,000 kwa siku, shilingi 20,000 kwa siku na kuna wodi za kawaida ambazo pia zimekarabatiwa kwa shilingi 12,000 kwa siku.
Wakati huo huo, Dkt. Rashid Mfaume alifanya ziara pia kukagua ujenzi katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo baada ya ukaguzi ameitaka Halmashauri kuendelea kukamilisha majengo yaliyobakia ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Dkt, Mfaume aliambatana na Wakurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Wilaya ya Bunda; maafisa kutoka TAMISEMI, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Manispaa ya Musoma na Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa