Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amefanya majumuisho ya ziara yake ya kikazi Mkoa wa Mara na kuupongeza Mkoa wa Mara kwa matumizi makubwa ya mfumo wa usimamizi wa Sekta ya Afya (GOTHOMIS)
Akizungumza katika majumuisho hayo, Dkt. Mfaume ameeleza kuwa kwenye matumizi ya GoTHOMIS kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Mkoa wa Mara unafanya vizuri sana ukilinganisha na mikoa mingine hapa nchini.
“Karibu vituo vyote tulivyotembelea katika Mkoa wa Mara vinatumia mgumo wa GoTHOMIS na baadhi ya sehemu wanatumia GoTHOMIS iliyoboreshwa baada ya Mkoa kutoa mafunzo kwa watumishi kuhusiana na mfumo mpya” amesema Dkt. Mfaume.
Aidha, Dkt. Mfaume ameupongeza Mkoa wa Mara kwa makusanyo ya damu salama ambapo Mkoa wa Mara ulifanikiwa kukusanya chupa 26,882 kwa mwaka 2023 na kuongoza kitaifa katika ukusanyaji wa damu.
“Makusanyo ya damu ni kwa mwaka 2023 ni sawa na asilimia 142 ya mahitaji ya damu kwa Mkoa wa Mara ambapo kwa mwaka Mkoa unahitaji chupa 18,976 kwa ajili ya matumizi kwa wagonjwa mbalimbali” amesema Dkt. Mfaume.
Aidha, amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kuhamasika kuchangia damu na kuwataka watumishi wa sekta ya afya kuendelea kuwahamasisha watu kuchangia damu.
Wakati huo huo, Dkt. Mfaume ameitaka Kamati ya Usimamizi wa Huduma za Afya (CHMT) ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kujitafakari na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha na kutapika katika Halmashauri hiyo kwa haraka kabla ya mlipuko huo kusambaa katika maeneo mengi.
Aidha, amesema kero nyingi katika utoaji wa huduma za afya zimepokelewa TAMISEMI kutoka katika Halmashauri hiyo jambo ambalo linaonyesha kuwa udhaifu katika usimamizi wa sekta ya afya katika Halmashauri hiyo na kuna mgawanyiko na hamna ushirikishwaji katika Halmashauri hiyo.
Dkt. Mfaume pia amekemea kitendo cha vituo vya kutolea huduma za afya kununua dawa na vifaa tiba kwa wazabuni bila kufuata utaratibu wa mshitiri uliowekwa kwa ajili ya kusambaza dawa na vifaa tiba pale Bohari ya Dawa (MSD) inaposhindwa kutoa dawa au vifaa hivyo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi ameeleza kuwa anatumaini kila mmoja amesikia kuhusu mapungufu na mafanikio ya Mkoa katika vipengele mbalimbali na kufanyia kazi kurekebisha mapungufu yaliyoonekana.
Aidha, Bwana Lusasi ameiomba Ofisi ya Rais –TAMISEMI kuusaidia Mkoa wa Mara kwa kutoa fedha zilizoombwa ili kukamilisha awamu ya kwanza ya Hospitali za Halmashauri zinazoendelea kujengwa katika Mkoa wa Mara ili ziweze kutoa huduma kwa wananchi.
Bwana Lusasi amesema japokuwa hospitali hizo kwa sasa zinafanyakazi, lakini zikiwezeshwa zitakuwa zinatoa huduma nyingi zaidi katika majengo yaliyopo wakati Serikali ikisubiriwa kuongeza majengo na kujenga walk way katika hospitali hizo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara, Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na Kamati za Usimamizi wa Sekta ya Afya (CHMT) wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na baadhi ya watumishi wa Mkoa na Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa