Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amefanya kikao cha majumuisho ya ziara yake Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Herieth uliopo katika Mji wa Bunda na kukipongeza Kituo cha Afya Magena, kilichopo Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt, Mfaume amesema kutokana na utendaji mzuri wa kituo hicho, huduma zimeboreshwa, makusanyo ya kituo ni makubwa na kuna ushirikiano mkubwa miungoni mwa watumishi jambo ambalo amesema linachangia mafanikio hayo.
“Kituo hiki kimeweza kulipa stahiki zote za wafanyakazi ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wenye ajira za muda 13 na kununua jenereta ya shilingi milioni 19 kutokana na mapato ya ndani ya kituo” amesema Dkt. Mfaume.
Aidha, amevitaka vituo vingine vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara kwenda kujifunza katika kituo hicho na hususan utaratibu wake wa kuwa na siku ya huduma kila siku ya Ijumaa kwa kila wiki na kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa uwazi kwa watu wote.
Dkt. Mfaume amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kuupongeza uongozi wa Kituo cha Afya Magena kwa barua na kuwapata motisha ya kufanyakazi vizuri na kuongeza ubunifu katika maeneo mengine ya utoaji wa huduma.
Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Tarime Mji kutoa shilingi milioni sita kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la mochwari katia kituo hicho na kuahidi kuwa Ofisi ya Rais- TAMISEMI italeta fedha za kujenga wodi katika Kituo cha Afya Magena ili kuboresha zaidi huduma za kituo hicho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Bibi Gimbana Ntavo ameeleza kuwa awali Halmashauri hiyo ilikuwa na wateja wengi wanaotoka nje ya Halmashauri lakini haikuwa inatoa huduma nzuri na vituo vya kutolea huduma za afya vilikuwa vinaitegemea Halmashauri kuvipa fedha za uendeshaji, menejimenti ikafanya utafiti wa namna ya kuboresha huduma za vituo hivyo.
“Baada ya utafiti, tuliangalia maeneo ya kuboresha na tukayafanyia kazi na sasa wingi wa wagonjwa umekuwa fursa kwetu, wagonjwa wanaridhika na huduma, mapato ya vituo yameongezeka kutoka shilingi milioni 290 hadi shilingi milioni 859 kwa mwaka” amesema Bibi Ntavo.
Bibi Ntavo amesema kwa sasa vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Mji wa Tarime vinaweza kujiendesha kwa mapato ya ndani ya vituo ikiwa ni pamoja na kuwaajiri na kuwalipa mishahara watumishi waliopata ajira za muda katika vituo hivyo.
Aidha, Bibi Ntavo amesema awali Halmashauri ilikuwa na changamoto ya ujazaji wa fomu za bima ya afya na vituo vingi ikiwemo Hospitali ya Halmashauri vilikuwa vinakatwa fedha na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa sasa Halmashauri imeajiri daktari kwa ajili ya kusimamia ujazaji wa fomu za bima na malipo ya bima hayakataliwi tena.
Bibi Ntavo ameipongeza Kamati ya Usimamizi wa Afya (CHMT) katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuboresha huduma za afya na makusanyo ya Serikali katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Aidha, Bibi Ntavo amesema Kituo cha Afya Magena kimekuwa kikifanya vizuri kwa muda mrefu na aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho amehamishiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ambapo pia ameboresha huduma katika Hospitali hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara, Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na Kamati za Usimamizi wa Sekta ya Afya (CHMT) wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na baadhi ya watumishi wa Mkoa na Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa