Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mara kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Magoma kabla ya Juni 30, 2020 ili kuhakikisha fedha iliyotolewa na serikali inatumika katika muda uliopangwa.
Akizungumza leo tarehe 20 Aprili katika ziara ya kukagua maendeleo ya kituo hicho, Mhandisi Nyamhanga ameeleza kuwa tayari serikali imetoa fedha yote ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho na sasa kinachobakia ni utekelezaji tu wa kazi za ujenzi.
“Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi milioni 500 tangia mwezi Desemba 2019 na mpaka sasa bado kuna kazi kubwa inahitajika kuweza kukamilisha kituo hiki” alisema Eng. Nyamhanga.
Aidha aliupongeza uongozi wa Mkoa kwa kuweza kukamilisha jengo la OPD ambalo limeanza kutumika kutoa huduma kwa wananchi wakati ujenzi wa majengo mengine ukiwa katika hatua mbalimbali.
Akijibu maombi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuhusu uhaba wa watumishi wa afya, Eng. Nyamhanga amesema anafahamu ikama ya Kituo cha Afya inataka kuwe na wafanyakazi 52 na kituo hicho kwa sasa kina watumishi wawili tu na kuahidi kuisaidia halmashauri kuleta wataalamu zaidi wa afya ili waweze kuletwa katika kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake Bwana Jackson Julius Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Magoma ambaye ni msimamizi mkuu wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Magoma, ameeleza kuwa mpaka sasa fedha iliyokwisha kutumika ni shilingi 220,936,243 kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo na zaidi ya shilingi 343,272,800 bado zipo banki.
Aidha ameeleza changamoto kubwa walioipata wakati huu wa mvua ni namna ya kuleta vifaa vya ujenzi katika eneo la ujenzi kutokana na ubovu wa barabara na mvua inayoendelea kunyesha. “Barabara ya kufika eneo hili ni mbovu sana na inatukwamisha sana katika shughuli za ujenzi” alisema Bwana Julius.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Dkt. Joseph Ngowi ameeleza kuwa awali kituo hicho hakikuwa katika bajeti ya dawa na vifaa tiba kwa mwaka huu wa fedha 2019/2020 lakini tayari Halmashauri imetenga bajeti katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 ambayo tayari imeshapitishwa na Bunge.
“Kwa kipindi hiki cha mpito, tumefanikiwa kupata vifaa tiba, dawa na watumishi wa kuanzia kutoa huduma katika kituo hiki kutoka katika vituo vya afya na zahanati zilizopo hapa wilayani” alisema Dkt. Ngowi.
Kituo cha Afya Magoma kilipokea awamu ya kwanza ya fedha kutoka serikalini mwaka 2018 ya kujenga jengo la OPD ambapo ujenzi wake umeshakamilika na kuanza kutoa huduma aidha kimepokea awamu ya pili ya fedha Desema 2019 na ujenzi wa majengo yake upo katika hatua mbalimbali.
Katibu Mkuu TAMISEMI yupo katika ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Mara kutembelea miradi mbalimbali na kukagua shughuli za maendeleo katika Wilaya za Tarime, Serengeti na Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa