Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mara kuboresha kiwango cha ufaulu katika mitihani ya taifa kwa shule za msingi na sekondari.
Eng. Nyamhanga ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti tofauti katika ziara yake ya siku tatu ya kutembelea Mkoa wa Mara na kukagua maendeleo katika sekta ya Elimu, Afya na utayari wa Mkoa katika kukabiliana na janga la homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
“Tumeiona mipango yenu na utekelezaji wake umeanza lakini tunahitaji ufaulu upande. Na sisi kwa upande wa wizara tumembadilisha Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara labda tutakuja kupata matokeo mazuri wakati huu” alisema Eng. Nyamhanga.
Katika kuunga mkono juhudi mbalimbali za wananchi na watendaji wa Mkoa wa Mara, Katibu Mkuu TAMISEMI aliahidi kutoa fedha za kusaidia ukamilishaji wa maboma ya madarasa, nyumba za walimu na maabara katika shule mbalimbali alizozitembelea katika ziara hiyo.
Katika ziara yake ya Mkoa wa Mara, Katibu Mkuu TAMISEMI alitembelea shule za sekondari za Kebogwe, Tarime na Nyamigwela na Shule ya Msingi ya Nyasaricho katika wilaya ya Tarime; Sekondari za Mapinduzi, Mugumu na Natta katika Wilaya ya Serengeti; na Sekondari ya Kabasa katika Wilaya ya Bunda.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula ameahidi Mkoa kufanya vizuri kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali pamoja na wadau wa Elimu katika Mkoa wa Mara.
“Kwa niaba ya watendaji wote wa Mkoa huu, tunashukuru sana wadau wetu mbalimbali ambao wamekuwa wakiunga mkono uboreshaji wa elimu katika Mkoa wa Mara” alisema Bibi Mthapula.
Katibu Mkuu TAMISEMI ametembelea wilaya za Tarime, Serengeti na Bunda katika Mkoa wa Mara kukagua shughuli za maendeleo katika sekta za Afya, Elimu na kuangalia utayari wa mkoa katika kukabiliana na janga la Korona.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa