Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara leo tarehe 28 Julai, 2022 imetoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake katika robo ya Aprili hadi Juni, 2022 na kueleza kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU imefuatilia utekelezaji wa miradi 24 ya maendeleo.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Antony Gang’olo, ameeleza kuwa miradi iliyofuatiliwa ilikuwa na thamani ya shilingi 18,578,309,485 katika sekta za afya, barabara, maji na elimu.
“Katika ukaguzi huo, miradi mitatu ilibainika kuwa na changamoto ambazo zinaendelea kurekebishwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa chumba cha wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime; mradi wa maji wa Kijiji cha Robanda na mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Sekondari ya Mapinduzi katika Wilaya ya Serengeti” alisema Gang’olo.
Aidha, Bwana Gang’olo ameeleza kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU imetembelea klabu za wapinga rushwa 86 katika Wilaya zote sita na kufanya mikutano ya hadhara 30 katika vijiji, mitaa na vitongoji mbalimbali katika Mkoa wa Mara.
Bwana Gang’olo ameeleza kuwa katika kipindi hicho pia TAKUKURU imeshiriki katika vikao 15 na kutoa mada za kuelimisha umma pamoja na kushiriki vipindi vitatu katika vituo vya redio za kijamii za Victoria FM, Mazingira FM na Bunda FM.
Wakati huo huo, Bwana Gang’olo ameeleza kuwa katika kipindi hicho, jumla ya malalamiko 106 na kati ya malalamiko hayo 79 yalihusu vitendo vya rushwa yanaendelea kufanyiwa kazi wakati 27 hayakuhusu vitendo vya rushwa.
“Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 26 yalihusu TAMISEMI, 11 Afya, 07 Jeshi la Polisi, 06 sekta ya vuvi, 06 sekta ya ardhi na sekta nyinginezo” alisema Bwana Gang’olo.
Bwana Gang’olo ameeleza kuwa katika kipindi hicho, uchunguzi katika majalada 18 ulikamilika na kesi 18 zilifunguliwa mahakamani na kufanya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa 36 huku kesi tatu zikiamriwa ambapo kesi 2 washtakiwa walipatikana na hatia na kesi moja mshtakiwa aliachiwa huru.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai- Septemba 2022 TAKUKURU Mkoa wa Mara itaongeza nguvu zaidi katika kuzuia vitendo vya rushwa na itashirikiana na Chama cha Skauti Tanzania kutekeleza mpango wa TAKUSKA unaolenga kutoa elimu ya rushwa kwa vijana wengi zaidi.
Taarifa hii ya TAKUKURU ni mwendelezo wa taarifa zinazotolewa na TAKUKURU Mkoa wa Mara kwa waandishi wa habari kila baada ya miezi mitatu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa