Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara leo imetoa taarifa yake ya utendaji kwa kipindi cha Januari, 2024 hadi Machi, 2024 ambapo imefuatilia miradi ya maendeleo 32 yenye thamani ya shilingi 11,372,416,636.5 inayotekelezwa na Serikali katika sekta za elimu, afya, barabara na maji.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Mohamed Shariff imeeleza kuwa uchunguzi wa awali ulibaini dosari katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara inayoendelea kujengwa katika Wilaya ya Bunda yenye thamani ya shilingi bilioni nne.
“Tayari Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imerekebisha dosari zilizoonekana ikiwa ni pamoja na kuta zilizokuwa zimepinda kwenye vyumba vya madarasa, nyufa kwenye mabweni, fundi amekatwa shilingi 360,000 kufidia simenti iliyotumika kutengeneza ukuta mnene uliozidi katika ujenzi wa bweni na vitabu vya stoo vilivyokuwa havijazwi kwa sasa vinajazwa” amesema Bwana Shariff.
TAKUKURU imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kuyafanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwa wakati hata hivyo uchunguzi wa kina kuhusiana na shule hiyo bado unaendelea.
Bwana Shariff ameeleza kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU ilipokea malalamiko 103, kati ya hayo malalamiko 57 yalihusu vitendo vya rushwa na 46 hayakuhusu vitendo vya rushwa na kesi moja ilifunguliwa mahakamani na kesi moja iliyokuwa mahakamani imeamriwa na Jamhuri kupata ushindi.
Aidha, TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mifumo ya utoaji na usimamizi ya adhabu katika Shule ya Sekondari ya Nyamunga katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya baada ya kupokea malalamiko ya kuwatoza wanafunzi wanaokamatwa na simu shilingi 200,000.
Bwana Shariff ameeleza kuwa katika kipindi hicho pia TAKUKURU imefanya uelimishaji umma kupitia klabu za wapinga rushwa 30 kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati, mikutano ya hadhara 31 na semina 20.
Kwa mujibu wa Bwana Shariff, mkazo uliwekwa katika uzuiaji wa vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utoaji wa huduma na kuwashirikisha wadau katika mapambano dhidi ya rushwa na jumla ya wananchi waliopatiwa elimu kuhusu rushwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara ni 6,220.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa