Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kupitia programu yake ya TAKUKURU Rafiki imesaidia Kijiji cha Seka kilichopo katika Kata ya Nyamrandirira, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kulipwa kwa deni la shilingi 37,500,000 kutoka katika mgodi wa MMG Gold Limited kwa ajili ya uwajibikaji wa jamii.
Akitoa taarifa ya robo ya kwanza kwa waandishi wa Habari, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara Bwana Mohamed Shariff leo tarehe 15 Novemba, 2024 amesema makubaliano kati ya mgodi huo na Kijiji cha Seka yalikuwa kila mwezi Kijiji kilipwe shilingi 1,500,000 kwa ajili ya kugharimia shughuli za utawala.
“Wakati kero hii inaibuliwa mgodi ulikuwa unadaiwa shilingi 40,500,000 ambazo zilikuwa hazijalipwa kwa muda wa zaidi ya miaka mitano, baada ya TAKUKURU Mkoa wa Mara kufanya ufuatiliaji mwekezaji amelipa shilingi 37,500,000 katika deni hilo” amesema Bwana Shariff.
Bwana Shariff amesema awali Mgodi wa MMG ulidai haukuwa na fedha za kulipa lakini baadaye ukalipa fedha hizo kwenye akaunti ya Kijiji cha Seka na Kata ya Nyamrandirira ambao ndio wanufaika wa fedha za uwajibikaji kwa jamii kwa mujibu wa mkataba uliopo baina ya Kijiji cha Seka na Mgodi wa MMG.
Katika hatua nyingine TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa na Serikali na kufanikiwa kudhibiti wizi wa mabati 104 yenye thamani ya shilingi 4,576,000 katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Chifu Sarota baada ya mzabuni kuwasilisha mabati 696 badaya ya mabati 800 yaliyonunuliwa.
Bwana Shariff ameeleza kuwa TAKUKURU imefuatilia miradi ya maendeleo 32 yenye thamani ya shilingi 43,550,103,153.23 katika sekta za afya, elimu, barabara na maji na kati ya hiyo miradi minne yenye thamani ya shilingi 655,159,402 ilikutwa na dosari na hatua zimechukuliwa miradi hiyo imerekebishwa.
Bwana Shariff amesema TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji wa mabaraza ya ardhi ya kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kubaini mabaraza hayo yakitoa hukumu katika mashauri ya ardhi badala ya kutekeleza mabadiliko ya sheria namba 3 ya mwaka 2021 inayotoa mamlaka ya kusuluhisha tu na sio vinginevyo.
“TAKUKURU iliwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambaye alitoa katazo kwa kuwaandikia barua Watendaji wa Kata kusitisha mabaraza hayo kutoa hukumu” amesema Bwana Shariff.
Bwana Shariff ameeleza kuwa TAKUKURU imefanikiwa kutoa elimu kupitia klabu za wapinga rushwa 56 kutoka shule za msingi, Sekondari na vyuo vya kati na mikutano ya hadhara 61, maonesho 9, vipindi vya redio vinne na semina 31.
Wakati huo huo, TAKUKURU Mkoa wa Mara imeendelea kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwaelimisha wadau wa uchaguzi na wananchi kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
Bwana Shariff amesema katika kipindi hicho wamepokea malalamiko 93 na kati ya hayo malalamiko 56 yalihusu rushwa, 37 hayahusu rushwa na kuongeza kuwa malalamiko ambayo yalikuwa hayahusu rushwa watoa taarifa walishauriwa sehemu sahihi ya kuyapeleka.
Aidha, TAKUKURU imeendesha jumla ya kesi 21 mahakamani ambapo kesi mpya ni tisa na kesi za zamani ni 12 na kesi saba zimeamuliwa ambapo Jamhuri imepata ushindi wa kesi sita na kesi moja imeondolewa mahakamani.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa