Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo ameipokea rasmi Programu ya TAKUKURU Rafiki kutoka kwa Kamanda wa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara Bwana Hassan Mossi kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya Programu hiyo, Mheshimiwa Mzee ameitaka TAKUKURU kuendelea kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara ili wananchi waweze kupata manufaa yaliyokusudiwa kutokana na miradi hiyo.
“Ninatamani kuona miradi ya maendeleo inayosuasua ikikamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata manufaa inayotokana na miradi hiyo na ninyi (TAKUKURU) mkifuatilia tutapata matokeo mazuri zaidi” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua kwa haraka kwa makosa ya uharifu ambayo yapo wazi ili kuleta matumaini kuhusu nia ya Serikali ya kukomesha matukio ya uhalifu.
Mheshimiwa Mzee pia ameipongeza kazi nzuri inayofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Mara na kuwataka kuendelea hususan katika utoaji wa huduma kwa wananchi wa vijijini na wasio na uwezo wa kulipia gharama za huduma.
Akizungumza wakati wa kuitambulisha Programu hiyo, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Hassan Mossi amesema TAKUKURU Rafiki inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bwana Mossi ameeleza kuwa kuanzia sasa, Maafisa wa TAKUKURU watatembelea maeneo mbalimbali katika Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Mara ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ushiriki wao katika kupambana na rushwa.
“Tutafanya vikao vingi hadi ngazi ya kata vya kutambua kero zinazowakabili wananchi kwenye utoaji na upokeaji wa huduma za afya, elimu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo wa miundombinu ya kutolea huduma” alisema Bwana Mossi.
Bwana Mossi amesema Programu hii inatarajiwa kusaidia kukuza utawala bora kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma na katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
TAKUKURU Rafiki ni programu inayotekelezwa kupitia Mpango Mkakati wa TAKUKURU kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2025/2026 na inalenga kupanua wigo wa kushirikisha wananchi na wadau katika kutambua na kutatua kero katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa