Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa Wa Mara leo imetoa taarifa kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara kuhusu shughuli walizozifanya katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2023 ambapo imekagua miradi 30 yenye thamani ya zaidi shilingi bilioni 12.4 katika sekta za afya, elimu, maji, barabara na utawala.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Fidelis Kalungura na kuwasilishwa kwa waandishi wa habari na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Antony Gang’olo imeeleza kuwa jumla ya miradi mitatu kati ya miradi yote iliyokaguliwa ilikutwa na dosari.
Miradi yenye dosari ni pamoja na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Buturi, Wilaya ya Rorya, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu matatu ya vyoo katika Shule ya Msingi Kamimange Wilaya ya Butiama na Ujenzi wa Kituo cha Afya Machochwe.
Bwana Gang’olo ameeleza kuwa katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Machochwe “mradi huu umejengwa chini ya kiwango, ununuzi wa vifaa vya ujenzi haukuzingatia mahitaji ambapo baadhi ya vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 6.2 vimebakia, ambayo ni hasara kwa serikali”.
Akizungumzia mradi wa Kituo cha Afya Machochwe, Bwana Gang’olo ameeleza kuwa mradi huo una viashiria vya rushwa na uchunguzi na tayari umeanzishwa.
Aidha katika mradi wa Shule ya Msingi Mamimange Wilaya ya Butiama, vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi 4,660,000 vilivyonunuliwa viliingizwa katika vitabu lakini havikupokelewa, hali ambayo imechelewesha kukamilika kwa mradi.
Bwana Gang’olo ameeleza kuwa katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Kidato cha tano na sita katika Shule ya Seondari Buturi, Wilaya ya Rorya, tofali 800 za shilingi 1,600,000 hazikuwa na ubora, TAKUKURU ilielekeza tofali hizo zisitumike katika ujenzi huo na ikawa ni hasara kwa mkandarasi.
Aidha taarifa hiyo imeonyesha kuwa TAKUKURU imefanya uelimishaji wa jamii kupitia njia ya uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa 62 za shule za msingi, Sekondari na vyuo vya kati; mikutano ya hadhara 48, semina 45 na imeshiriki katika maonesho tisa na jumla ya watu walioelimishwa katika kipindi hicho ni 9247.
Aidha Bwana Gang’olo ameeleza kuwa jumla ya malalamiko 128 yamepokelewa katika kipindi hicho na kati ya malalamiko hayo, 76 yalihusu vitendo vya rushwa, 52 hayakuhusisha vitendo vya rushwa na malalamiko yote yameshughulikiwa.
Aidha, mashtaka mapya 3, jumla ya kesi 20 ziliendeshwa katika mahakama mbalimbali katika Mkoa wa Mara ambapo kesi 12 zilitolewa maamuzi na upande wa Jamhuri ilishinda kesi sita na kesi sita washtakiwa waliachiwa huru.
Taarifa hii ni mwendelezo wa utaratibu wa kawaida wa TAKUKURU kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu yake katika kira baada ya miezi mitatu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa