Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kuchunguza na kuwachukulia hatu wote waliohusika katika ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Manga iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Agosti 2021 wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
“Yoyote atakayekuwa amehusika kwa namna moja au nyingine katika hasara hii ya fedha za wananchi achukuliwe hatua za kisheria na mhakikishe kuwa fedha hizi zinarudi na wanafunzi wanapata bwalo haraka iwezekanavyo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo baada ya kushuhudia kuta za bwalo la chakula zikiwa zimepinda na kuezuliwa baada ya jengo hilo kujengwa kwa kutumia nondo za milimita 12 badala ya milimita 16 iliyokadiliwa kwenye BOQ.
Akiwa shuleni hapo Mheshimiwa Hapi amekagua ujenzi wa madarasa na kukemea utaratibu wa kutumia mirango ya mabati kwenye vyumba vya madarasa na nyumba za watumishi badala ya milango ya mbao ambayo ni salama zaidi.
Mheshimiwa Hapi ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kujenga vyoo vya wanafunzi ndani ya miezi sita ili kuwapunguzia adha wanafunzi wanaokaa bweni kutumia matundu machache ya vyoo ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo.
Mkuu wa Mkoa pia akiwa shuleni hapo ameivuja Kamati ya Shule ya Sekondari ya Manga kutokana na usimamizi mbovu wa bwalo hilo na kuisababishia serikali hasara.
Mheshimiwa Hapi akiwa shuleni hapo ameonyeshwa bweni moja lililojengwa kwa nguvu za wananchi miaka 17 iliyopita na Halmashauri imeshindwa kukamilisha ujenzi huo na kuagiza jengo hilo likamilishwe ndani ya miezi sita.
Awali akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Shule hiyo Bi. Editha Nakei ameeleza kuwa ujenzi wa bwalo hilo umetumia zaidi ya shilingi milioni 96 na ulitekelezwa kwa mfumo wa force account.
Bi. Nakei ameeleza kuwa awali fundi aliyekuwa anajenga jengo hilo alisimamishwa lakini walipokea maelekezo kutoka Halmashauri kuwa fundi aendelee na kazi ya ujenzi.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye na viongozi wengine wa chama na serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa