TAKUKURU KUCHUNGUZA MIRADI YA CSR TARIME
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kuchunguza miradi inayotekelezwa kutokana na fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika vijiji 11 vinaouzunguka mgodi huo.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Agosti 2021 wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
“Yoyote atakayekuwa amehusika kwa namna moja au nyingine katika ufujaji wa fedha za wananchi achukuliwe hatua za kisheria mara moja, awe amehama, awe amestaafu au awe amefukuzwa waitwe kujibu mashtaka yao” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea miradi mine inayotekelezwa kwa kutumia fedha za CSR na kukuta matumizi mabaya fedha, miradi kutekelezwa chini ya kiwango na kutokukamilika kwa muda mrefu pamoja na fedha ya mradi kutolewa na mgodi mapema.
Miradi hiyo ni ujenzi wa Shule ya Msingi Tarajali ya Ntimaro ambapo yamejengwa madarasa sita na kila darasa limegharimu shilingi milioni 26 huku likiwa halijawekewa vigae, umeme, dari halijafungwa gypsum, viti, meza na limeanza kupasuka kabla ya kutumika.
Aidha katika shule hiyo zimejengwa nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa kuchukua familia mbili kila mmoja kwa gharama ya shilingi milioni 77 kila nyumba mmoja.
“Matumizi haya ni makubwa mmno na yamepitiliza viwango ambavyo kwa mawaida tunatekeleza miradi ya serikali lakini ubora wa kazi hii pia ni wa hovyo hovyo tu haijafanyika vizuri” alisema Mheshimiwa Hapi.
Katika mradi wa ujenzi wa maabara ya Kituo cha Afya cha Nyangoto, maabara hiyo imejengwa kwa gharama ya shilingi 110 na tangu mwaka 2019 mpaka sasa bado haujakamilika. Aidha katika utekelezaji wa mradi huu, matofali yalinunuliwa mara mbili ya mahitaji yake na hivyo mengi yamebakia huku yakinunuliwa kwa shilingi 2,500 kwa tofali tofauti na bei ya soko.
Katika mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa vya shule ya Sekondari ya Matongo, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 80 na umekamilika lakini madarasa hayatumiki kwa sababu hayana viti na meza wakati nondo 900 kati ya nondo zilizonunuliwa kujenga mradi huo zimebakia bila matumizi.
Aidha katika mradi wa ujenzi wa barabara wanannchi wamelalamikia ubora wa barabara hiyo lakini Meneja wa Mamlaka za vijijini na Mijini (TARURA) ameeleza kuwa barabara hiyo imejengwa kwa mujibu wa viwango vinavyohitajika.
Mhehsimiwa Hapi amewakumbusha watumishi wote wa serikali kutimiza majukumu yao kwa weredi maana serikali imelipa madeni, kuongeza watumishi, kupunguza kodi na kuwapandisha madaraja; watumishi nao wapandishe madaraja ya utendaji wao.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Hapi ameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye maarufu kama Namba Tatu, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Diaz Ndomba, viongozi na watendaji wa Wilaya ya Tarime na baadhi ya taasisi za serikali za Mkoa wa Mara.
Ziara ya Mheshimiwa Hapi ilianza tarehe 9 Agosti 2021 ambapo alitembelea wilaya ya Serengeti kwa siku mbili na leo ameanza ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa siku mbili na baada ya hapo ataendelea na ziara yake katika Hamashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa