Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kuchunguza matumizi ya fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazotolewa na Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori (WMA) katika vijiji vitano vya pori la akiba la Ikoma pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 10 Agosti 2021 katika nyakati tofauti baada ya kubaini kuwa ndani ya miaka mitano vijiji hivyo vimepewa shilingi bilioni 4.1 na pesa hizo kutumika katika miradi ambayo haijatekelezwa vizuri.
“Ninataka uchunguzi wa kina wa vijiji hivi ili tuweze kubaini matumizi ya fedha hizi za CSR na wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na ufisadi pamoja na uzembe uliofanyika hapa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Katika miradi hiyo Mheshimiwa Hapi amekuta matumizi ya fedha ni makubwa ikilinganishwa na kazi iliyofanyika, baadhi ya miradi haijakamilika na fedha zimeisha, baadhi ya miradi kutengenezwa chini ya viwango na kadhalika.
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakuu wa Vitengo na Idara pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kutimiza wajibu wao kwa weredi na ufanisi ili kuendelea kubakia katika utumishi na nyadhifa hizo.
Aidha amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bwana Kivuma Khamis Msangi kusimamia utendaji wa watumishi na kuvunja makundi yote yaliyokuwepo awali.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa WMA Bwana Yusuph Manyanda ameeleza kuwa jumuiya yake imekuwa ikitoa fedha kulingana na makusanyo yake ya mwaka kwa serikali za vijiji vinavyoizunguka jumuiya hiyo.
“Mwaka 2017/2018 tulitoa milioni 298; 2018/2019 tulitoa shilingi milioni 262; 2019/2020 tulitoa milioni 193 na mwaka 2020/2021 tulitoa shilingi milioni 81 kwa kila kijiji” alisema Bwana Manyanda.
Bwana Manyanda ameeleza kuwa juma ya fedha iliyopelekwa kwenye vijiji hivyo kama fedha za uwajibikaji kwa jamii ni shilingi bilioni 4.1 ambapo vijiji vilitumia fedha hizo kutekeleza miradi mbalimbali waliyoamua kuitekeleza chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wialaya ya Serengeti.
Aidha Bwana Mayanda ameeleza kuwa fedha hizo zilikuwa zikitolewa kila mwaka na kuanzia mwaka jana imepungua kutokana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19 katika sekta ya utalii hapa nchini.
Amevitaja vijiji vinavyohusika katika tukio hilo ni vijiji vya Park Nigoti, Robanda, Makundusi, Nichoka na kijiji cha Ikoma.
Mheshimiwa Hapi leo ameendelea na ziara yake katika siku ya pili ambapo ametembelea miradi wa ujenzi wa madarasa, maji na bwalo la chakula na kuzungumza na wananchi katika Shule ya Sekondari ya Robanda; mradi wa maji katika Kijiji cha Makundusi; kufanya mkutano na wananchi katika eneo la omahe,
Aidha Mheshimiwa Hapi ametembelea Shule ya Sekondari ya Makundusi na kuzungumza na viongozi mbalimbali na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti katika Shule ya Sekondari ya Nuru iliyopo katika mji wa Mugumu.
Kesho Mheshimiwa RC ataendelea na ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo atakagua kwa siku mbili.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa