Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene leo anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku nne katika Mkoa wa Mara ambapo atakagua na kutembelea miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, baada ya kupokelewa Mhe. Simbachawene anategemewa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, kuzindua vyumba 13 vya madarasa, matundu 17 ya vyoo na mabweni matano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe, kuzindua daraja katika Mtaa wa Majengo Mapya kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Sekondari Mara, Manispaa ya Musoma.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa kesho Mhe. Simbachawene anatarajiwa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kuzindua Shule ya Sekondari ya Ingri na kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Utegi Wilaya ya Rorya.
Msafara utaelekea Wilaya ya Tarime, ambapo Mhe. Simbachawene atazindua Shule ya Msingi Komote na mradi wa maji Kemakorere na baadaye kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Kemakorere.
Tarehe 3 Oktoba, 2024 Mhe. Simbachawene anategemea kuzindua Zahanati ya Getarungu na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Getarungu, kuweka jiwe la msingi katika barabara ya Stendi Mpya katika mji wa Mugumu, Wilaya ya Serengeti.
Baada ya hapo msafara unatarajiwa kuelekea Wilaya ya Butiama ambapo Mhe. Simbachawene anatarajiwa kuzindua Shule ya Msingi ya chifu Manyori na kufanya mkutano wa hadhara katika stendi ya mabasi katika eneo la Nyamisisi.
Tarehe 4 Oktoba, 2024 Mhe. Simbachawene anatarajiwa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Zahanati ya Nambaza, kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara na kuzindua Shule ya Sekondari ya Bunda Mjini kabla ya kuhitimisha ziara hiyo na mkutano wa hadhara katika eneo la Stendi ya Zamani iliyopo katika Mji wa Bunda.
Mhe. Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, lililopo katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma katika ziara hii anatarajiwa pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa