Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene leo tarehe 2 Oktoba, 2024 amefanya ziara katika Wilaya ya Tarime ambapo ameipongeza Wilaya ya Tarime kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hiyo baada ya kuzindua Shule ya Msingi Komote na mradi wa maji katika Kijiji cha Kemakorere na kuridhika na utekelezaji wa miradi hiyo.
“Hapa katika shule hii, shilingi milioni 540 zilizotumika zinaonekana kwa macho ya kila mtu, awali nilijua ni shule ya sekondari kumbe ni shule ya msingi” amesema Mhe. Simbachawene na kuipongeza Serikali kwa maamuzi yake ambayo yamepunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Nkende.
Mhe. Simbachawene ameipongeza Serikali kwa kujenga shule mpya katika eneo hilo na kuongeza kuwa hapo awali, isingekuwa rahisi kwa Serikali kutoa fedha zote za kujenga shule mpya kwa mara moja kutokana na bajeti iliyokuwa inatengwa, lakini kwa awamu ya sita inawezekana.
Akizungumzia kuhusu mradi wa maji wa Kemakorere Mhe. Simbachawene ameipongeza Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) kwa mradi huo ambao unatoa huduma ya maji kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Mhe. Daniel Komote ameishukuru Serikali kwa kujenga shule hiyo nay eye kama Diwani wa Kata hiyo aliwahamasisha wananchi ambao wamechangia baadhi ya shughuli katika kuingiza maji, umeme na kulima barabara ya kuingilia katika shule hiyo.
Mhe. Komote amesema wananchi pia wanachangia chakula cha wanafunzi shuleni na wanafunzi wote wa shule hiyo wanakula shuleni na kuwalipa walimu sita wanaojitolea katika shule hiyo kutokana na upungufu wa walimu.
Mhe. Komote amesema kutokana na mwanzo mzuri katika ushirikiano wa wazazi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo, anategemea shule hiyo itafanya vizuri kutokana na msingi mzuri uiojengeka baada ya kuanzishwa kwake.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa