Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene leo amefanya ziara Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuwahamasisha wananchi wa eneo la Suguti kufanya uwekezaji ili kuuendeleza Kijiji hicho kuwa Mji wa Suguti.
Mhe. Simbachawene amesema hayo wakati akiwasalimia wananchi wa eneo la Suguti na kuongeza kuwa Serikali imeshajenga barabara ya lami na kuweka majengo ya ofisi mbalimbali za Serikali katika eneo hilo na kulifanya eneo hilo kuwa mji na kuwataka wananchi kujenga nyumba za kupangisha na kuanzisha biashara kwani wateja wameongezeka.
“Eneo hili halifai tena kuwa kijiji bali Mji, hapa ni makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na mali kubwa mliyonayo wananchi katika eneo hili ni ardhi mliyonayo na mnaweza kuiuza au kuiendeleza”amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuyapima maeneo ya wananchi ili kuupanga mji katika eneo hilo kwa maandalizi ya kuwa mji na kuanza kuwekeza katika kujenga nyumba za watumishi kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri.
“Kukiwa na nyumba za watumishi hapa, watumishi wengi watapenda kuishi hapa na hii itasadia mzunguko wa fedha na kurahisisha uwekezaji katika eneo hili” amesema Mhe. Simbachawene.
Kuhusu upungufu wa watumishi, Mhe. Simbachawene amesema kuwa watumishi wa sekta za elimu na afya wapo katika hatua nzuri za kuajiriwa baada ya Serikali kutoa vibali vya ajira na mchakato wa ajira hizo kufanyika kupitia Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa.
Mhe. Simbachawene amewahimiza wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Simbachawene ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.5.
Akitoa taarifa za ujenzi wa hospitali hiyo, Mkuu wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Dkt. Joseph Fwoma amesema katika hospitali hiyo tayari majengo 16 yamejengwa na kufikia katika hatua mbalimbali.
Dkt. Fwoma amesema hospitali hiyo ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 87 ambapo kwa sasa Hospitali ina watumishi 40 kati ya watumishi 312 wanaohitajika.
Dkt. Fwoma amesema Hospitali hiyo kwa sasa imeanza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI, maabara, wagonjwa wa dharura, mama na mtoto, tohara, kulaza wagonjwa, lishe, kliniki ya mkoba, kinywa na meno na ustawi wa jamii.
Dkt. Fwoma amesema Hospitali hiyo inapokea wagonjwa wa malipo ya papo kwa papo, wagonjwa wa msamaha na wagonjwa wanaotumia bima za afya na kuongeza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika Hospitali hiyo asilimia 92.
Katika ziara hiyo, Mhe. Simbachawene ameongozana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalam ya Wilaya ya Musoma, viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Wakuu wa Idara na Vitengo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa