Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuimarisha usimamizi katika utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 14 Agosti 2021 wakati akizungumza na wananchi, viongozi na watumishi katika maeneo tofauti tofauti kazita ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo.
“Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya huduma za jamii ili wananchi waweze kupata huduma hizo katika maeneo yao bila usumbufu wa kusafiri muda mrefu, simamieni huduma hizo zipatikane” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amezitaja huduma ambazo wananchi wanahitaji ziimarike kwa haraka ni elimu, afya, maji, barabara, umeme na ulinzi wao na mali zao.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kwa upande wa elimu, serikali na wananchi wameleta fedha za kujenga miundombinu, serikali imewapandisha madaraja walimu, imeajiri walimu wapya wa masomo ya sayansi ili kuimarisha elimu.
“Sasa kazi yetu ni kuhakikisha maboresho haya makubwa ambayo serikali imeyafanya katika sekta ya elimu yaonekane kwenye matokeo ya mitihani ya wanafunzi, na hayo yatawezekana tu endapo wanaohusika wakisimamia ufundishaji na kudhibiti utoro wa wananfunzi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha katika sekta ya afya, serikali imeongeza miundombinu, bajeti ya dawa, vifaa tiba na kuongeza wataalamu wa afya pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi waliokuwa wanastahili.
“Sasa halmashauri ni jukumu lenu kusimamia uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi, udhibiti wa wizi wa dawa na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika sehemu zao ili waweze kufanyakazi vizuri” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mheshimiwa Juma Chikoka kusimamia utendaji wa taasisi zilizo katika wilaya yake ambazo zinamajukumu ya kutoa huduma maji, umeme, barabara na kadhalika kwa wananchi.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya Bwana Valentine Deogratius Maganga ameeleza kuwa zama zimebadilika, kwa sasa wananchi wanahitaji maendeleo.
“Sasa sio wakati wa watumishi kukaa maofisini na kuongea tu muda wote, wananchi hawa wanaidai serikali maendeleo ambayo yanapatikana baada ya wataalamu kuyasimamia kwa weredi” alisema Bwana Maganga.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa