Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka viongozi wa wilaya na wataalamu wa afya kusimamia utekelezaji wa mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na watoto kuhusu udhibiti wa UVIKO-19.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 27 Julai 2021 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Mwongozo ule unamambo mengi mazuri na ya msingi yakisimamiwa tutaweza kupunguza sana kuenea kwa maambukizi ya UVIKO -19 katika mkoa wetu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amesema kwa mfano mwongozo unataka harusi ziahirishwe au kama zitafungwa ziwe na watu wachache, zifanyike maeneo ya wazi na shughuli yote ifanyike ndani ya muda mfupi.
Mheshimiwa Hapi amesema sehemu za biashara zote ziwe na tahadhari za UVIKO 19 ikiwemo maji tiririka ya kunawa, vitakasa mikono, kuzingatia ukaaji kwa nafasi na uvaaji wa barakoa.
“Mkoa wa Mara tupo mpakani tunatakiwa kuongeza juhudi katika udhibiti kwa sababu tupo mpakani na maeneo yetu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amewataka wataalamu wa afya kutoa elimu kuhusu chanjo ili itakapofika wananchi watakaoridhia waweze kuipata katika vituo vitakavyobainishwa.
Mkuu wa Mkoa amewataka wataalamu wa afya kutekeleza maelekezo ya serikali kuhusiana na idadi ya watu wanaoenda hospitali kuangalia wagonjwa, utoaji wa matibabu na hususan dozi kwa watu wenye magonjwa ya muda mrefu.
Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mara Bi. FLowina Muuzaje ameeleza kuwa chanjo zinatarajiwa kuzinduliwa tarehe 28 Julai 2021 na zinatarajiwa kutolewa bure kwa wananchi watakaoridhia kuchanjwa.
Bi. Muuzaje ameeleza kuwa japokuwa ukichanjwa unaweza kupata tena maambukizi ya UVIKO-19 lakini nguvu ya ugonjwa huo inakuwa imepungua baada ya kupata chanjo kuliko kabla ya chanjo hiyo.
“Chanjo hizi ni salama na zimepitishwa na wataalamu wa afya duniani na zinauwezo wa kupunguza athari za UVIKO- 19 kwa watu wengi zaidi kuliko kabla ya kupata chanjo” alisema Bi. Muuzaje.
Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) ya Mkoa wa Mara pamoja na mambo mengine kimejadili masuala ya lishe na jitihada za udhibiti wa UVIKO- 19 katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa