Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata ambao shule zao zilifanya vibaya kwenye Somo la Kiingereza katika mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2023 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti leo tarehe 27 Novemba, 2023 wamepewa mafunzo ya namna ya kusimamia ufundishaji wa somo hilo yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Azimio A.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Mujibu Mustafa Babara ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu na kuwataka washiriki wa mafunzo kufuatilia mafunzo hayo ili kwenda kubadilisha hali ya ufundishaji wa somo hilo.
“Tunataka mkimaliza mafunzo hayo, mabadiliko ya wazi yaonekani kwa namna walimu wenu watakavyokuwa wanafundisha na namna wanafunzi watakavyoongeza ufaulu wa asomo la kiingereza katika shule zenu” amesema Bwana Babara.
Bwana Babara ameeleza kuwa kwa Mkoa wa Mara wataalamu hao watakuwa wakwanza kupewa mafunzo ya kusimamia na kutekeleza muhutasari wa somo la Kiingereza kwa shule za Msingi kulingana na Mtaala wa Elimu ya Msingi, 2023.
“Ninyi mnapewa mafunzo kwenye mada mpya kabisa ambayo nina uhakika sio walimu wote hapa nchini watapata fursa mliyoipata leo, tuyatendee haki haya mafunzo na tukawajibike katika kuwasimamia walimu wanaofundisha” amesema Bwana Babara.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Bwana Sam Mwita ameeleza kuwa ufaulu wa somo la Kiingereza kitaifa ni asilimia 34 na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ilikuwa ni ya mwisho katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, 2023.
“Ni mategemeo yetu kuwa mafunzo haya, na mafunzo yatakayotolewa kwa waliu kesho yataboresha ufundishaji wa wanafunzi na hivyo kuja kuboresha matokeo ya somo la kiingereza katika mitihani ya ndani na mitihani ya Taifa” amesema Bwana Mwita.
Bwana Mwita ameelezea imani yake kuwa walimu hao wanaouwezo wa kufanya mabadiliko na wanasifa za kufanya mabadiliko na kuwataka kutekeleza kwa ufanisi mpangokazi watakaotoka nao katika mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mdhibiti Ubora wa Kanda ya Ziwa Bibi Lucy Nyanda ameeleza kuwa kuna mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu na hivyo walimu hawana budi kujifunza kuhusu mtaala na sera mpya za elimu zilizoanza kutumika hivi karibuni.
Bibi Nyanda amewataka washiriki hao kuchukulia mafunzo hayo kama chachu ya kujifunza mambo yote yanayohusiana na elimu na mabadiliko ya mitaala na sera ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mafunzo ya Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu Kata yanatarajiwa kufuatiwa na mafunzo kwa walimu wanaofundisha somo la Kiingereza katika shule hizo yanayotarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 28 Novemba, 2023.
Mafunzo haya yanatolewa na Wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM) na kufadhiliwa na Mradi wa Shule Bora.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa