Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amezungumza na viongozi wa wananchi wa eneo la Ghuba ya Speke, katika Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda na kuwataka wananchi kuwashirikisha viongozi wa Serikali changamoto zao ili waweze kusaidiana kuzitatua.
Mheshimiwa Mungiya ameeleza hayo wakati akizungumza na viongozi wa wananchi wa Kata ya Nyatwali katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo ofisini kwa Mkuu wa Mkoa na kumuomba awasaidie ili wanapoondoka katika eneo la Ghuba ya Speke wapate fidia wanazostahili na na walipwe mapema ili waweze kuendelea na majukumu yao mengine.
“Sisi viongozi tupo hapa kwa ajili yenu, tukishirikiana mambo yote yaawezekana ikiwa ni pamoja na mambo magumu ambayo tunaweza kudhani hayawezekani lakini tukiweka nguvu zetu kwa pamoja yote yanawezekana” amesema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewashukuru viongozi hao kuja kuzungumza nae na kuwataka kuwasiliana nae kama kuna changamoto nyingine yoyote itakayowapata wakati wa utekelezaji wa utwaaji wa eneo la Nyatwali.
Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi hao kuwaelimisha wananchi wa Nyatwali kuhusiana na umuhimu wa wao kushirikiana na wathamini wakati wa kufanya uthamini wa maeneo na mali zao ili waweze kulipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.
Taarifa ya viongozi hao iliyosainiwa na Diwani wa Kata ya Nyatwali Mheshimiwa Mashimo Malongo kwa niaba ya wananchi wa Nyatwali, imeeleza kuwa wananchi wa Nyatwali wameomba Serikali kutoa nyongeza ya fidia ili wananchi watakaohamishwa waweze kujikimu baada ya kuhamisha kwa hiari katika eneo hilo.
“Wananchi wa Kata ya Nyatwali hawapingani na Serikali na wala hawakatai kuhama lakini wanamashaka juu ya fidia watakayolipwa ili kupisha uendelezaji wa eneo hilo” na kuongeza kuwa kufuatia ziara ya Mawaziri wa Kisekta katika eneo hilo, wananchi wamehamasika kuchukua fomu za utambuzi na kuthaminishwa kwa ardhi na mali wanazomiliki.
Wakizungumza na Mkuu wa Mkoa, viongozi hao wameiomba Serikali kuwalipa fidia ya ardhi sawa na bei ya ardhi inayouzwa na Halmashauri ya Mji wa Bunda ambako wengi wao wataenda kununua maeneo baada ya kuhamisha kutoka katika Kata ya Nyatwali.
Mapendekezo mengine ni pamoja na Serikali kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu ukokotoaji wa majengo; wameomba nyongeza ya malipo ya makaburi kukidhi gharama halisi za kuhamisha makaburi; nyongeza ya fidia za mazao ya chakula, mazao ya biashara na miti; fidia za mali zisizohamishika; wapewe fidia ya usumbufu (Disturbance allowance); gharama za kuanzia makazi; fidia ya kusafirisha mifugo; fidia ya vyoo; na fidia ya vyombo vya uvuvi.
Viongozi hao wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuhakikisha utwaaji wa eneo hilo unafanyika kwa amani na utulivu wakati wote wa zoezi la uthamini, ulipaji wa fidia na uhamaji wa wananchi.
Viongozi waliokutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara ni pamoja na Diwani wa Kata ya Nyatwali, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Nyatwali, Wenyeviti wa Mitaa ya Tamau, Serengeti, Nyatwali na Kariakooo na wananchi wanne waliowawakilisha wenzao kutoka katika mitaa ya Kata ya Nyatwali.
Serikali imeamua kulitwaa eneo la Ghuba ya Speke, katika Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengati na kulinda usalama wa wananchi wa eneo hilo ambalo lipo kandokando ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ziwa Victoria.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa