Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo (16 Februari, 2024 amefungua mafunzo ya siku moja ya Maafisa biashara, Tehama na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Mara kuhusu mfumo wa kuwatambua na kuwasajiri wafanyabiashara wadogo yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma.
Akizungumza katika halfa ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Bwana Makungu amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga mazingira wenzeshi ya wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) kufanya biashara zao ili kujipatia kipato kwa maendeleo yao na jamii kwa ujumla.
“Tangu nchi yetu ipate uhuru, kwa mara ya kwanza Serikali ya awamu ya sita inajenga ofisi kila Mkoa kwa ajili ya viongozi wa chama cha wafanyabiashara wadogo hapa nchini na inaanzisha mfumo rasmi wa kuwatambua na kuwasajiri kama kundi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu amewataka wataalamu watakaohusika kuwatambua na kuwasajiri wafanyabiashara wadogo kufanyakazi hiyo kwa umakini na kwa uzalendo ili kutoa nafasi kwa walengwa wa kundi hili kutambuliwa kiurahisi.
Bwana Makungu ameeleza kuwa mfumo huu umekuja ili kuboresha mfumo wa awali wa utoaji wa kuwatambua na kuwahudumia wafanyabiashara wadogo hapa nchini kutokana na umuhimu wa kundi hilo kwa maendeleo ya nchi yetu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Biashara na Viwanda Bwana Timotheo Gambaless ameeleza kuwa mfumo huo wa kielekroniki utawezesha kupata taarifa za utambulisho wa uraia, taarifa za watu wa karibu na mfanyabiashara huyi na aina ya biashara na sehemu biashara inapofanyika.
Bwana Gambaless ameeleza kuwa katika mfumo huu mpya wafanyabiashara watalipia shilingi 20,000/= kama awali lakini kitambulisho atakachopatiwa kitatumika eneo lolote hapa nchini bila kuhitaji kujisajiri tena.
Aidha, Mfumo huu utakapokamilika utaiwezesha Serikali kuwatambua na kufuatilia taarifa mbalimbali za wafanyabiashara wadogo hapa nchini na kufuatilia maendeleo yao na namna wanavyokua kibiashara hadi kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Mafunzo haya ya siku moja yameendeshwa na Wizara ya Viwanda na Biashara na kuhudhuliwa na maafisa Tehama, Biashara na Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa