Serikali imewashauri wananchi wa Nyamongo hususan vijiji 11 vinaouzunguka Mgodi wa Barrick North Mara kubadilika ili kuweza kufaidi fursa za maendeleo zinazoletwa na kuwepo kwa mgodi katika eneo hilo.
Kauli hiyo imetolewa na viongozi mbalimbali leo tarehe 20 Mei wakati wa uzinduzi wa ulipaji wa fidia kwa wananchi 1639 wa vijiji viwili vya Nyamongo katika Wilaya ya Tarime ambao ardhi yao imechukuliwa na mgodi huo.
Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko amewataka wananchi wa Nyamongo kubadilika ili kuweza kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na mgodi huo.
“Kuwepo kwa mgodi hapa ni fursa kubwa sana kwenu ambayo ikitumiwa vizuri maisha yenu pia yatabadilika sana” alisema Mheshimiwa Biteko.
Ameeleza kuwa ili kuweza kufaidika na fursa za mgodi huo, wananchi wanatakiwa wafanye uzalishaji wa chakula, mifugo na mahitaji mengine ya mgodi kwa ubora na uwingi unaotakiwa na hapo serikali itawasaidia kupata soko kwenye mgodi huo.
Aidha amewaagiza viongozi wa Mgodi wa Barrick North Mara kuhakikisha kuwa maisha ya wananchi wa Nyamongo yanaendana na mgodi ili kuweza kupunguza vurugu na manung’uniko kutoka kwa wananchi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu amewatahadharisha wafaidika wa fidia hiyo kuhusu uwezekano wa kuibiwa fedha zao na kuwashauri waziwekeze kwenye shughuli za maendeleo.
“Kwa sasa watu wanajua mmepata pesa, mtapata marafiki wengi na wakila aina, lakini sio wote hao wanania nzuri” alisema Mheshimiwa Zungu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka wananchi hao kutumia fedha hizo ili kuanzisha miradi ya maendeleo.
“Haiwezekani fedha zote hizi zije hapa leo halafu tubakie hivi hivi hata akija mgeni baadaye asione ukumbusho wa fedha hii, tuwekeze kwenye vitu vya maana na tuubadilishe mji wetu” alisema Malima.
Alisema kwa sasa Nyamongo ina tawi la Benki ya NMB na sasa Benki ya CRDB imeahidi kufungua tawi ndani ya mwezi mmoja.
“Ukiona mabenki yanafungua matawi yake hapa Nyamongo ujue tayari pametambulika kama sehemu ya kiuchumi” alisema Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa njia kubwa ya kubadilika ni kuondokana na migogoro inayowafaidisha watu wengine na kujipanga ili kuleta maendeleo yao.
“Kila kunapokuwa na mgogoro kuna watu wengine wamekuwa wakifaidika, lakini safari hii serikali imechukua hatua stahiki na kutatua mgogoro huu na sasa mnalipwa fidia” alisema Malima.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bibi Angelina Mabula amewaasa wananchi wa Nyamongo na maeneo mengine nchini kuacha tabia ya kutegesha katika maeneo ambayo miradi inapita ili kurahisisha maendeleo yao.
“Hii tabia ya kutegesha ni mbaya sana, watu mnapanda miti au kujenga katika maeneo ambayo tathmini inaendelea au imeshakamilika ili kulipwa fidia na hivyo kuchelewesha malipo ya fidia kwa wate wanaohusika” alisema Mheshimiwa Mabula.
Uzinduzi wa malipo ya fidia kwa wananchi wa Nyamongo ulihudhuriwa na Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angelina Mabula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo na viongozi wengine wa Serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa