Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameendelea na ziara yake katika Wilaya ya Serengeti na kutembelea Kijiji cha Mbalibali ambapo amefanya mkutano wa hadhara na kikao cha wadau wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
“Kama wote tunakiri kuwa hifadhini kuna hatari nyingi na wote hatujui kwa nini wenzetu hawarudi wakiingia huko, tunakwenda kufanya nini huko? Kwa nini linakuwa suala la kawaida kwenda sehemu ambayo tunajua ina hatari na baadaye tunalalamika?” Amesema Mhe. Mtambi
Akiwa katika mkutano wa Hadhara Mhe. Mtambi amewataka wananchi wanaoingia SENAPA kuacha mara moja tabia hiyo kwani ndani ya hifadhi hiyo kuna wanyama wakali, majangili na nyoka wa kila aina ambao wanaweza kuwadhuru na kupoteza maisha.
Kanali mtambi amezungumzia upotoshaji uliopo katika jamii kwa kutoa tafsiri za upotoshaji na hususan miungoni mwa vijana ambazo amesema wakati mwingine zina madhara makubwa na kutolea mfano kila mtu anayepotea katika maeneo hayo kusemekana ameuawa na askari wa SENAPA bila ushahidi wowote.
Mhe. Mtambi amekemea wananchi kueneza hadhithi za kutisha kuhusu hifadhi na maafisa wa hifadhi ya SENAPA bila ya kuwa na ushahidi kwa kuwa ameeleza kwa mtu anayeingia hifadhini anaweza kupatwa na mambo mengi kulingana na hali halisi iliyopo hifadhini.
Akizungumza na wazee na wadau wa uhifadhi, Mhe. Mtambi amewataka kukemea vikundi vya watu na wanasiasa ambao wanapotosha jamii kwa kutoa matamko yanayopingana na Serikali hata katika mambo ya maendeleo kama uhifadhi wa SENAPA.
“Hawa watu wanaweza kuwa wanatumika na wasioitakia mema nchi yenu na kuwafanya wao kuwa mawakala wa kujimaliza wao wenyewe kwa kufifisha juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo Watanzania” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amemtaka Mkuu wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuyatembelea mahoteli yaliyopo hifadhini na kuyaomba ajira kwa vijana katika hoteli hizo ili kutengeneza ajira kwa vijana wanaozunguka SENAPA.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti Bwana Japan Mrobanda amewataka wananchi kufuata maelekezo ya Serikali ili kuilinda SENAPA kwa maendeleo yao na Tanzania kwa ujumla.
“ Serikali ya CCM inataka watu wote tuishi kwa amani, tuheshimiane na tupendane na tuishi kwa umoja na amani. Kuishi kando kando ya Serengeti sio dhambi, mshukuruni Mungu kwa hilo dhambi ni kutumia vibaya ukaribu wako na hifadhi”. Amesema Bwana Mrobanda.
Bwana Morobanda ameeleza kuwa CCM muda wote inawapigania wananchi ili waweze kuona matunda ya hifadhi kwa kuwekewa huduma muhimu za kijamii, lakini baadhi ya wananchi wanavichafulia vijiji na hivyo kukosa sifa za kupata uwekezaji kutoka TANAPA.
Bwana Morobanda aliishauri Serikali kutafuta timu za wazee wa mila ili kuzungumza nao wasaidie juhudi za Serikali kukomesha ujangili katika hifadhi ya SENAPA.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji ameeleza kuwa Mkuu wa Mkoa amefika eneo hilo kwa ajili ya kujitambulisha, kusikiliza kero zao na kuzungumza nao kuhusiana na mambo mbalimbali.
Dkt. Mashinji amewataka wananchi kuacha kuifuata SENAPA na kuingia ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ya kufanya shughuli za kibinadamu na kuwashawishi “waisusie” hifadhi hiyo kwa muda waone kama hifadhi itawafuata walipo wao.
Katika vikao hivyo, wananchi wameomba Serikali iwaletee barabara, maji, umeme, malambo ya mifugo, mabweni katika shule kulinda wananfunzi dhidi ya wanyama wakali na mito kujaa maji wakati wa mvua na kupatiwa ajira katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Katika mikutano hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamatiya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti na Menejimenti ya Wilaya ya Serengeti, maafisa kutoka SENAPA, TAWA na TANAPA na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, taasisi na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa