Serikali ya Mkoa wa Mara imewataka wafugaji kufuga kisasa na kuboresha mifugo yao ili kuwawezesha kupata soko la uhakika la mifugo na mazao ya mifugo yao ili kuboresha uchumi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi iliyosomwa kwa niaba yake na Mhe. Moses Kaegele, Mkuu wa Wilaya ya Butiama katika uzinduzi wa Nyama Choma Festival iliyofanyika katika mnada wa Kiabakari Wilaya ya Butiama.
“Wafugaji wakifuga kisasa watasaidia kupata mifugo iliyo bora na nyama bora ambayo itawawezesha kupata soko la uhakikika kwa ndani na nje ya nchi” amesema Mwalimu Kaegele.
Mhe. Kaegele amesema Mkoa wa Mara unayo mifugo mingi ambayo ikitumika vuzuri itakuza uchumi wa wananchi na Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla na kuwataka wananchi kuchangamkia ufugaji wa kisasa wa mifugo.
Mwalimu Kaegele ameeleza kuwa mashindano hayo ni endelevu na yameanza katika Wilaya ya Butiama na yatafanyika katika Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara lengo likiwa kuwapata wachoma nyama mahiri ambao watatumika katika kuchoma nyama katika matukio mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Mara.
“Mkoa utayatumia mashindano haya kuwatangaza wachoma nyama mahiri waliopo katika Mkoa wa Mara ili waweze kutumika katika matukio mbalimbali ya ndani na nje ya Mkoa katika matukio mbalimbali” amesema Mhe. Kaegele.
Mhe. Kaegele amewataka wananchi kudumisha amani, utulivu na usalama ili kuweza kuwavutia watu zaidi wengi zaidi kushiriki katika mashindano hayo na kuwekeza katika Wilaya ya Butiama kufuatia Serikali kuanzisha Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Technolojia (MJNUAT) Butiama ambacho kinategemewa kuanza kudahili wanafunzi 4,000 kwa mwaka hivi karibuni.
Bwana Kaegele ameeleza kuwa uwekezaji unaohitajika zaidi ni mahoteli, mabweni ya wanafunzi, nyumba na usafiri kwa ajili ya ongezeko kubwa la idadi ya watu linalotegemewa baada ya ujenzi wa Chuo hicho kukamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama Mhe. Christopher Marwa Siagi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yakifanyika vizuri yanaweza kuutangaza Mkoa wa Mara kwa namna ya kipekee.
Mhe. Siagi ameeleza kuwa tukio hilo limepata mwitikio mkubwa japokuwa linafanyika kwa mara ya kwanza na kutangazwa ndani ya muda mfupi ni kutokana na umuhimu wake kwa wajasiriamali na mahitaji halisi ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
Mashindano hayo yamehudhuriwa pia na Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Butiama, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Butiama, baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, taasisi za umma zilizopo Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa