Serikali imetoa vifaa vya maabara vya masomo ya Kemia, Fisikia na Biolojia kwa shule za sekondari 1258 hapa nchini vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano ili kuinua kiwango cha elimu hususani masomo ya sayansi hapa nchini.
Akizungumza leo tarehe 20 Aprili 2020 wakati wa kukagua vifaa vya maabara vilivyoletwa katika Shule ya Sekondari ya Kebogwe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema tayari vifaa hivyo vimeshasambazwa na kuanza kutumika katika shule mbalimbali hapa nchini.
“Huu ni uwekezaji mkubwa sana kwa serikali katika sekta ya elimu, na lengo ni kuinua ufundishaji wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari hapa nchini” alisema Eng. Nyamhanga.
Eng. Nyamhanga ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2020/2021 iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, TAMISEMI imepanga kutoa fedha za ujenzi wa maabara saba za sayansi kwa kila halmashauri hapa nchini ili kuendeleza jitihada za kuinua ufundishaji wa masomo ya sayansi.
Wakati huo huo, Eng. Nyamhanga ameahidi kuwa TAMISEMI itatoa fedha za kukamilisha ujenzi wa Jengo la Utawala na nyumba ya walimu katika Shule ya Sekondari ya Kebogwe.
Akizungumza baada ya kukagua shule hiyo na kupokea taarifa ya shule, Eng. Nyamhanga amesema “serikali itaunga mkono juhudi za wananchi ambao wamejenga majengo hayo na wameshindwa kuyamalizia”.
Aidha ameipongeza shule hiyo kwa kuendelea kuboresha taaluma ingawa bado ina changamoto ni nyingi ikiwemo za miundombinu ya kujifunzia na kufundishia na nyumba za walimu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Kebogwe ameeleza kuwa shule hiyo ilianza mwaka 2015 kwa kujengwa kwa nguvu za wananchi. Mpaka wakati huu shule ina jumla ya wanafunzi 333 wa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Ameeleza kuwa idadi ya wanafunzi imekua ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Shule ilianza ikiwa na wanafunzi 37 wa kidato cha Kwanza lakini mpaka sasa, shule ina wanafunzi 104 wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2020.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa