Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mheshimiwa Dkt. Suleiman Jafo leo amepokea matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya Kitaifa iliyokuwa inachunguza uchafuzi katika Mto Mara.
Akiwasilisha taarifa ya uchunguzi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Samwel Manyele ameeleza kuwa uchafuzi wa Mto Mara umetokana na nguvu za asili na shughuli za binadamu katika eneo oevu la Mto Mara.
Prof. Manyele ameeleza kuwa katika eneo oevu la Mto Mara lenye ukubwa wa kilomita za mraba 423 kumekuwa na shughuli za kibinadamu ambazo ni kilimo na ufugaji.
“Katika eneo hili kulikuwa na ng’ombe zaidi ya laki tatu waliokaa hapo kwa zaidi ya miezi nane na hadi wakati uchunguzi unafanyika bado kuna ng’ombe kiasi pamoja na ushahidi kuwa wakati wa kiangazi watu huwa wanaishi katika eneo hilo oevu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa kiangazi wafugaji wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanaweka ng’ombe wao katika eneo hilo oevu kwa ajili ya malisho na maji ya mifugo jambo ambalo limesababisha uwepo wa mlundikano wa kinyesi, mkojo pamoja na maozea ya uoto wa asili wa mto huo.
“Kulikuwa na kiwango kikubwa cha uozo wa mimea, kinyesi, mikojo ya wanyama kilichokuwa kimerundikana katika eneo uevu na kingo za Mto Mara kwa muda mrefu lakini mto umechafuka wakati huu kutokana na uozo huo kutibuliwa na mvua kubwa zilizokuwa zinanyesha katika eneo hilo” alisema Prof. Manyele.
Profesa Manyele ameeleza kuwa hali ya maji kuwa meusi katika Mto Mara itaendelea kuwa hivyo kwa muda wa miezi mitatu hadi minne kama mvua kubwa haitanyesha tena kusafirisha kwa haraka uozo huo.
Taarifa ya Kamati hiyo inaonyesha kuwa maji ya Mto Mara na maji ya visima kuzunguka eneo la Mto Mara ni salama na hayawezi kuathiri afya za binadamu wanayoyatumia maji hayo.
Profesa Manyele ameeleza kuwa taarifa waliyoipata kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara imeonyesha kuwa katika kipindi hiki kulikuwa hamna magonjwa ya binadamu yaliyotokana na matatizo ya maji.
Hata hivyo Kamati hiyo imeeleza kuwa picha zilizokuwa zimesambazwa mitandaoni kuonyesha samaki wengi wakiwa wanaelea sio za Mto Mara wala Ziwa Victoria bali ni picha za maeneo mengine.
“Katika kutafuta sampuli ya samaki tumezunguka na boti kwa siku mbili kutafuta waliokuwa wamekufa kwa ajili ya uchunguzi katika eneo hilo” alisema Prof. Manyele.
Profesa Manyele ameeleza kuwa uchunguzi wao ulihusisha pia mahojiano ya watu mbalimbali ikiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimba madini, wananchi wanaoishi kando kando ya Mto Mara na wataalamu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Jafo ameipongeza kamati hiyo kwa kazi nzuri walioifanya pamoja na taasisi zote zilizoshiriki kwa hali na mali katika kufanikisha uchunguzi huo kufanyika kwa kina na kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Jafo ameitaka Kamati hiyo kuwasilisha taarifa kamili ya uchunguzi ndani ya siku mbili ikiwa na mpangokazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati hiyo.
“Mpangokazi utasaidia katika utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa hiyo ili kila mamlaka ya serikali ipewe eneo lake na lilifanyie kazi kwa haraka” alisema Mheshimiwa Jafo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Mamlaka ya Maji na Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Mamlaka zote za Maji za Mkoa wa Mara kuweka mkakati wa kutibu maji kulingana na mapendekezo ya kamati ya wataalamu.
Aidha, Mheshimiwa Hapi amewapongeza viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kwa ustahimilivu na uvumilivu kwa kipindi chote ambacho kulikuwa na tatizo hilo.
Uchunguzi huo ulikuwa na lengo la kubaini chanzo cha uchafuzi wa Mto Mara uliopelekea rangi ya maji ya Mto kuwa meusi, kutoa harufu mbaya na viumbe hai ikiwemo Samaki kufa na kuelea juu ya maji kuanzia katika Kijiji cha Parasipora kilichopo katika Kata ya Bisumwa, Wilaya ya Rorya na Kijiji cha Wegero Kata ya Buswahili katika Wilaya ya Butiama.
Kamati hiyo iliongozwa na Prof. Samwel Manyele, kutoka Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Katibu wa Kamati hiyo ni Dkt. Samuel G. Mafwenga, Mkurugenzi Mkuu, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Wajumbe wa kamati hiyo ni Dkt. Kessy F. Kilulya, Mkuu wa Idara ya Kemia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Charles Kasanzu, kutoka Idara ya Jiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bwana Daniel Ndio, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali, Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Bwana Renatus Shinhu, Mkurugenzi wa Bonde, Mamlaka wa Bonde la Maji Ziwa Victoria.
Wajumbe wengine kuwa ni Bi. Baraka Sekadende, Mkurugenzi wa Kituo, Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), Mwanza, Dkt. Neduvoto Mollel, kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Usimamizi wa Viatilifu (TPHPA), Afisa kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Bwana Yusuf Gobe Kuwaya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Faraja Ngelageza, Mkurugenzi Msaidizi Bioanuai, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa