Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 13 Julai, 2022 ametoa mrejesho wa maamuzi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kuhusu fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Akizungumza katika kikao cha Baraza Maalum la Madiwani la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa maamuzi ya Waziri Mkuu yalitolewa katika kikao cha pamoja kilichowahusisha viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali, Mbunge wa Tarime Vijijini na viongozi wa Mgodi wa Barrick North Mara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa maamuzi ya kikao hicho yalikuwa fedha zote za CSR zinazotolewa na mgodi huo ni mali ya umma na matumizi ya fedha hizo lazima yafuate taratibu zote za fedha za Serikali za mitaa.
“Serikali imeamua kuwa hakutakuwa tena na Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyokuwa ikitumika kupanga na kutekeleza miradi ya CSR katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na badala yake miradi yote itatekelezwa kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya kawaida ya serikali” alisema Mheshimiwa Hapi.
“Wataalamu watapata fursa ya kuchambua miradi iliyoibuliwa na kufanya michakato ya kitaalamu kuhusiana na miradi hiyo kabla ya kuiwasilisha kwenye mamlaka za maamuzi kwa ajili ya kuidhinisha utekelezaji wa miradi hiyo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mfumo wa malipo ya fedha hizo itakuwa sawa na fedha zote za Serikali na zitapelekwa kwenye Kata ambapo mradi unatekelezwa na taratibu zote za fedha na manunuzi ya umma zitafuatwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa kuanzia sasa Serikali kwa maana ya Mkoa na Halmashauri utashiriki kwenye kukokotoa kiwango cha CSR kitakacholipwa na mgodi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime sio kama ilivyokuwa awali halmashauri ilikuwa ikipatiwa taarifa tu na mgodi kuhusu kiasi cha CSR.
Aidha, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa fedha ya CSR itatolewa kwa Dola za Kimarekani na Halmashauri ndio itakayehusika katika kubadilisha dola hizo kuwa fedha za kitanzania kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri.
“Huu utaratibu wa matumizi ya CSR umekubalika kuwa ni utaratibu wa nchi nzima baada ya kikao kilichofanyika chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Maamuzi haya ya Serikali yanahitimisha malumbano ya matumizi ya fedha CSR katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime yaliyodumu kwa muda mrefu kufuatia uongozi wa Mkoa wa Mara kuingilia kati matumizi ya fedha hizo na kuunda kamati maalum ambayo iliwasilisha taarifa yake tarehe 20 Aprili, 2022.
Hata hivyo kulikuwepo na malalamiko ya wananchi na wanasiasa hususan baada ya kuvunjwa kwa CDC tarehe 20 Aprili, 2022 na vyombo vya dola kuanza uchunguzi kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za CSR za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa