Serikali imetaifisha kilo 27.5 za madini ya dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na gari aina ya Toyota Harrier mali ya Bwana Barwesh Gandecha Mkazi wa Jiji la Mwanza yaliyokamatwa katika eneo la Sirari katika Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara.
Akizungumaza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ambaye pia ni Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Bwana Biswalo E. K. Maganga ameeleza kuwa mbali na kutaifisha mali hizo, Bwana Gandecha pia amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni 315.
“Hukumu hiyo imetolewa jana tarehe 15 Juni 2020 na Hakimu Veronica Mgendi wa mahakama ya Wilaya ya Tarime baada ya Bwana Gadencha kufikishwa mahakamani na kukiri makosa ya utakatishaji wa fedha na umiliki wa madini kinyume cha sheria” alisema Bwana Maganga.
Ameeleza kuwa Bwana Gandecha alikamatwa katika mji wa Sirari Mei 15, 2020 akiwa na dhahabu hiyo ambayo awali alidanganya kuwa aliingiza nchini ikitokea nchi jirani ya Kenya lakini hakuwa na nyaraka za kuonyesha kuwa madini hayo yalitokea nchini Kenya.
Bwana Maganga ameeleza kuwa uchunguzi umebaini kuwa dhahabu hiyo imepatikana kupitia mtandao haramu unaofadhiliwa na Bwana Gandecha na kuwa alijaribu kutafuta nyaraka kwa njia ya udanganyifu ili kuweza kuhalalisha umiliki wa madini hayo.
“Uchunguzi pia umebaini kuwepo kwa watumishi wa serikali katika taasisi za umma ambao walikuwa wanamsaidia Bwana Gadecha kutengeneza nyaraka za kuhalalisha umiliki wa madini hayo na taratibu za kisheria zinafuatwa juu ya watumishi hao waliohusika” alisema Bwana Maganga.
Kwa mujibu wa Bwana Maganga serikali imetaifisha jumla ya kilo 425 za dhahabu katika kipindi cha miaka mitano tangu serikali ianze kutaifisha madini yanayomilikiwa kinyume cha sheria.
Akizungumza katika kikao hicho kati ya DPP na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa mtu huyo alikamatwa na vyombo vya dola kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya vyombo hivi katika Mkoa wa Mara na wananchi ambao waliamua kutoa taarifa juu ya umiliki wa madini hayo bila kufuata sheria.
“Ninawashukuru sana kwa ushirikiano huu na niwaombe wote wanaotaka kufanya biashara ya madini katika Mkoa wa Mara kufuata sheria na taratibu ili mfanye biashara yenu kihalali bila kubughudhiwa na mtu” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa ufanyaji wa biashara ya madini kwa njia halali utawasaidia wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa tija na kuwapatia maendeleo endelevu ambayo yatawanufaisha watanzania wote ambayo ndio nia ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa