Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga ametangaza rasmi kuongeza muda wa maonyesho kwa siku mbili baada ya tarehe 8 Agosti 2020 ili kutoa muda zaidi kwa wananchi kujifunza.
Mheshimiwa Hasunga ametoa maelekezo hayo leo tarehe 4 Agosti 2020 asubuhi katika viwanja vya Nyakabindi wakati anaongea na waandishi wa habari katika banda la Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA).
“Nimeona tutoe muda zaidi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kuendelea kujifunza zaidi teknolojia mbalimbali za kilimo zinazoonyeshwa katika maonyesho haya” alisema Mheshimiwa Hasunga.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Hasunga, maonyesho haya ya kilimo yakitumika vizuri wananchi wanaweza kujifunza zaidi kuhusu kilimo bora na namna ya kupata mikopo ya kuwekeza katika shughuli za kilimo kutoka katika taasisi za kifedha.
Nyongeza ya muda inawahusu waonyeshaji katika kanda zote nane ambazo zinaendelea na maonyesho yake katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, Lindi na Simiyu.
Wakati huo huo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Mwita Waitara amezikumbusha halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Waitara ameeleza hayo katika kikao cha majumuisho baaya ya kufanya ziara katika maonyesho ya nanenane katika viwanja vya Nyakabindi, Simiyu ambapo alikuwa mgeni rasmi kwa siku ya leo tarehe 4 Agosti 2020.
“Vijana ndio sehemu kubwa ya nguvu kazi ya nchi hii na ajira kubwa kwa hivi sasa ni kilimo na hawa hawana maeneo ya kulima, hivyo ni wajibu wa halmashauri kutenga maeneo ambayo yatatoa ajira kwa vijana” alisema Mheshimiwa Waitara.
Aidha aliahidi TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kilimo ili kuweza kuboresha kilimo hapa nchini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa