Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe leo amefunga mafunzo ya watumishi wa sekta ya afya ya namna ya kuwahudumia Mama na Mtoto na kuwahimiza watumishi hao kutumia teknolojia katika kuokoa maisha ya wagonjwa na hususan Mama na Mtoto.
Akizungumza na watumishi hao kutoka vituo 37 vya kutolea huduma za afya Mkoa wa Mara, Dkt. Magembe amesema matumizi ya teknolojia na hususan simu za mkononi zikitumika vizuri zinaweza kusaidia sana kuokoa maisha ya watu na hasa wanaohitaji huduma za dharura.
“Simu zinaweza kutumika katika kuomba msaada, kuuliza wazoefu na kueleza changamoto ya dharura iliyopo ili kuweza kupata ufumbuzi wa tatizo na kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa hususan wanaohitaji huduma za dharura” amesema Dkt. Magembe.
Aidha, amewataka waratibu wa mafunzo hayo kufanya mafunzo kama hayo nchi nzima na watumishi watakaopata mafunzo hayo waachwe watoe huduma za Mama na Mtoto ili ujuzi uliopatikana uweze kutumika kutatua changamoto za wananchi.
Aidha, amezitaka Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao ili kuwajengea uwezo na kuwapa uzoefu watumishi hao kuboresha huduma zao na kupunguza rufaa zisizo za razima.
Dkt. Magembe amesema kwa sasa hamna sababu ya wajawazito kupoteza maisha wakati na baada ya kujifungua kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya ikilinganisha na zamani.
Ametolea mfano zamani kulikuwa na vyumba vya wagonjwa mahututi vya watoto wachanga (Neonatal ICU) vine tu nchi nzima lakini hadi mwaka huu vipo 189 hapa nchini na vyote vinavifaa tiba na watumishi maalum kwa ajili ya huduma hizo.
“Kwa sasa hamna Mkoa wenye changamoto za vyumba vya wagonjwa mahututi vya watoto na katika baadhi ya mikoa vyumba hivyo vipo hadi ngazi ya Hospitali za Halmashauri” amesema Dkt. Magembe.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya 110 kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa mafunzo hayo ya wiki mbili kwa watumishi yanaweza kupunguza vifo vya watoto chini ya siku 28 baada ya kuzaliwa na vifo vinavyotokana na uzazi katika Mkoa wa Mara.
“Mkoa wa Mara unachangamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi, baadhi ya watumishi waliopo hawana ujuzi na uzoefu wa kuwahudumia wajawazito na watoto wachanga, upungufu wa vifaa tiba kwenye baadhi ya vituo vya kutolea huduma na wananchi kuchelewa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma wakati wa kujifungua”amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa kwa mwaka 2023 Mkoa wa Mara ulipoteza jumla ya wanawake 49 kutokana na uzazi kati ya vizazi hai 103,478 na vifo vya watoto wachanga chini ya siku 28 vilikuwa 766 kati ya vizazi hai 103,478 .
DKt. Masatu ameeleza kuwa sababu kubwa iliyochangia vifo vinavyotokana na uzazi ni kuvuja damu nyingi kabla na baada ya kujifungua na kwa watoto wachanga ni tatizo la kushindwa kupumua, matatizo yanayotokana na mtoto kuzaliwa njiti na vifo vinavyotokana na matatizo ya Mama wakati wa uchungu.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa kiwango cha wajawazito walioanza kliniki mimba chini ya wiki 12 kimeongezeka kutoka asilimia 38.4 mwaka 2022 hadi 46.6 mwaka 2023 na kiwango cha wajawazito waliohudhuria kliniki mara nne au zaidi imeongezeka kutoka asilimia 116.4 mwaka 2022 hadi 117 mwaka 2023.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa kwa mwaka 2023 Mkoa wa Mara ulipoteza jumla ya wanawake 49 kutokana na uzazi kati ya vizazi hao 103,478 na watoto wachanga chini ya siku 28 vilikuwa 766 kati ya vizazi hai 103,478 .
DKt. Masatu ameeleza kuwa sababu kubwa iliyochangia vifo vinavyotokana na uzazi ni pamoja na kuvuja damu nyingi kabla na baada ya kujifungua na kwa watoto wachanga ni tatizo la kushindwa kupumua, matatizo yanayotokana na mtoto kuzaliwa njiti na vifo vinavyotokana na matatizo ya Mama wakati wa uchungu.
Kwa upande wake, Muuguzi Mkunga kutoka Kituo cha Afya Murangi Bwana Musa Yohana ambaye ni kati ya wanufaika wa mafunzo hayo amesema kuwa kutokana na mafunzo hayo wamepata ujuzi, maarifa na uzoefu kutoka kwa wataalamu wabobezi na wanategemea wataboresha utendaji wao baada ya mafunzo.
Aidha, Bwana Yohana amesema kutokana na kuboreka kwa huduma katika Zahanati na Vituo vya Afya wanategemea rufaa za kwenda Hospitali za Halmashauri na Hospitali ya Rufaa zitapungua sana maana wagonjwa watapatiwa huduma stahiki kwenye vituo.
Ameishukuru Serikali kwa kuleta mafunzo hayo kwa wauguzi, wakunga na madakatari wanaowahudumia Mama na Mtoto.
Ufunguzi wa mafunzo hayo umehudhuriwa na Maafisa kutoka Wizara ya Afya, Kamati ya Usimamizi wa Afya ya Mkoa (RHMT), Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, wanganga wakuu wa Halmashauri, wakufunzi wa mafunzo na watumishi kutoka vituo 37 vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa