Serikali imepanga kutenga maeneo ya uchimbaji na kuwagawia vijana wa eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime ili waweze kujitafutia kipato cha halali kama sehemu ya kukabiliana na uvamizi wa mara kwa mara wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde amesema hayo wakati wa ziara yake na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni katika mkutano wa hadhara na wananchi wanaouzunguka mgodi huo uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Nyabigena, eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hataki kuona vijana wakiendeleza kuhangaika na kujihusisha na uvamizi mgodini na ameamua kuwapa maeneo ya uchimbaji na Serikali itawasaidia kuanza kuchimba ili kuwasaidia kutimiza malengo yao katika maisha” amesema Mhe. Mavunde.
Mhe. Mavunde ameeleza kuwa Wizara ya Madini imeweka mkakati wa kuyatumia maeneo ambayo leseni za uchimbaji wa madini zimefutwa kuwapatia vijana ili waweze kujiendeleza katika uchimbaji wa madini na kukuza kipato chao.
Mhe. Mavunde ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupeleka mitambo ya kuchoronga madini katika eneo la Nyamongo litakalotengwa kwa ajili ya vijana ili kuongeza tija kwenye uchimbaji katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amekemea vijana kuvamia mgodi huo na kuliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya amani na usalama katika maeneo yao.
Aidha, Mhe. Masauni amesema Serikali haifurahii kuona wananchi wanafariki wanapovamia mgodi huo na kulitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha Polisi Jamii katika eneo hilo na kuwachukulia hatua wananchi watakaokamatwa wakivamia mgodi na kuvunja mtandao wa uhalifu unaovamia mgodi huo.
Mhe. Masauni amewataka askari wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu na kumpongeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya kwa kuwachukulia hatua askari sita ambao wamehusika na matukio ya kutokufuata misingi ya kisheria katika kutekeleza majukumu yao eneo hilo.
Mhe. Masauni amewataka wananchi wa eneo la Nyamongo kufuata sheria za nchi na kuacha kuvamia mgodi na kuwashambulia askari wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao katika ulinzi wa mgodi huo, wanannchi na mali zao.
Katika Mkutano huo wananchi wa eneo hilo pia walipewa nafasi ya kutoa maoni, kero na changamoto zinazowakabili na Serikali kutoa majibu ya hoja hizo isipokuwa iliyohusu mgawanyo wa fedha za CSR kwa sababu suala hilo lipo mahakamani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde wamefanya ziara Mkoa wa Mara katika Wilaya ya Tarime kuelekea katika mgogoro kati ya wananchi na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Kabla ya kukutana na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi, Mawaziri hao walifanya kikao na Kamati ya Usalama ya Mkoa katika ukumbi wa uwekezaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Kamati ya Usalama Wilaya ya Tarime katika Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa