Uwekezaji katika upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Musoma unaofanywa na serikali ya unalenga kuubadilisha mji wa Musoma kuwa mji wa Utalii na Mkoa wa Mara kuwa ndio lango kuu la kuingilia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo tarehe 11 Septemba 2020.
“Uwanja wa ndege wa Musoma utakapokamilika utaleta ndege za Shirika la Ndege la Tanzania na ndege nyingine ambazo zitaleta watalii kwa wingi hususan katika msimu wa watalii” alisema Mheshimiwa Malima.
Amewahamasisha wafanyabiashara kuwekeza zaidi katika huduma za kuwahudumia watalii ili uwanja utakapokamilika kuwe na huduma za kuwapa watalii.
Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na chakula, mahoteli, mabenki, hospitali, usafiri, na kadhalika ambazo zitawafanya watalii kufurahia kuwepo Tanzania na hivyo kutamani kurudi tena.
Aidha amewataka wakazi wa Mkoa wa Mara kubadilisha mtazamo wao na kuanzisha ukarimu kwa wageni ili waweze kufaidika na fursa za utalii zilizomo katika Mkoa wa Mara.
“Mara ndio sehemu pekee ambapo Serengeti inakutana na Ziwa Victoria, wanyama wanapovukia kwenda Masai Mara, Kenya, Nyumbu wanapozaliana na kadhalika, tukiendelea na tabia zetu mbaya zitawatisha watalii na tutabakia kuwa nyuma kimaendeleo” alisema Malima.
Aidha amehimiza uwekezaji katika miji mingine ya Mugumu, Bunda na Natta ili kuweza kuwapokea na kuwahudumia watalii wanaotegemewa kuja baada ya uwanja wa ndege kukamilika Musoma.
Mheshimiwa Malima alisema Rais ametoa ahadi ya kukamilisha uwanja huo kutokana na umuhimu wake kwa Mkoa wa Mara lakini pia kwa ukuaji wa sekta ya utalii hapa nchini.
Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya kukamilisha uwanja wa ndege wa Musoma tarehe 5 Septemba 2020 katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Mukendo katika Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa