Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kupunguza athari za moshi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo salama kwa kuboresha upatikanaji na uhamasishaji wa wananchi kupikia nishati mbadala ambayo ni salama ili kulinda afya zao.
Hayo yameelezwa leo tarehe 11 Julai, 2022 na Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba ambaye amefanya ziara ya siku moja katika Mkoa wa Mara ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 21, katika mikoa 14 na Wilaya 38 hapa nchini iliyoanza leo.
“Tunataka tuwasaidie wananchi wengi wapikie nishati mbadala ambayo ni salama kwa matumizi ili waweze kuboresha maisha yao na afya zao” alisema Mheshimiwa Makamba.
Mheshimiwa Makamba ameeleza kuwa wananchi wanapata matatizo ya kiafya na hata kufa taratibu kutokana na matumizi ya mara kwa mara ya nishati ambazo zinahatarisha maisha yao bila wao kujua, “serikali tumeliona hili na tunachukua hatua” alisema Mheshimiwa Makamba.
Mheshimiwa Makamba ameeleza kuwa kwa Tanzania asilimia 72 ya nishati inayozalishwa inatumika viwandani na asilimia ndogo sana inatumika majumbani na hiyo inayotumika nyumbani inatumika zaidi katika kuwasha taa, kupooza vitu, kupiga pasi na kiasi kidogo sana kwenye kupikia.
Ameeleza kuwa asilimia 85 ya watanzania wanapikia nishati ya mkaa, kuni, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama jambo ambalo linahatarisha afya zao kutokana na moshi ambao ni sumu unaotokana na nishati hiyo ndio maana serikali ya awamu ya sita inataka mabadiliko kwenye nishati mbadala ya kupikia.
Mheshimiwa Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (Tanga) ameahidi kufunga mfumo wa majiko ya gesi katika eneo linalotumiwa na akina mama wa kikundi cha kukaanga dagaa cha Mwisenge (Musoma) na Shule ya Sekondari ya Makongoro (Bunda) ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kutumia nishati ya gesi kupikia.
Katika ziara hiyo pia Mheshimiwa Makamba amegawa mitungi midogo ya gesi ya kupikia ya kilo kwenye kikundi cha wananwake mwisenge na mtungi mmoja kwa ajili ya Bibi Tereza Stephano na kuahidi kumwekea umeme Bibi Tereza Stephano ambaye anatoka katika kaya maskini katika Wilaya ya Butiama.
Kwa upande wake uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara imeeleza kuwa inapokea wagonjwa 400 hadi 500 kwa mwaka wanaougua magonjwa mbalimbali yanayotokana na madhara ya moshi wa kuni, mkaa, sigara na vyanzo vingine kwa binadamu.
“Magonjwa yanayotokana na moshi yanaathiri watu wengi sana lakini hayapewi kipaumbele kwa sababu dalili za magonjwa haya huonekana baada ya mgonjwa kuathirika na moshi kwa muda mrefu katika kipindi cha miaka 15-20 au zaidi ya hapo” alisema Dkt. Mary Mahenge Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
Dkt. Mahenge ameeleza kuwa chanzo cha moshi huo ni pamoja na uvutaji wa sigara, kuni na mkaa, sigara wakati wa kupika na dalili za waathirika wa magonjwa yanayotokana na moshi ni pamoja na kutoa makohozi mazito, wanashindwa kulala vizuri na kubanwa na kifua mara kwa mara.
Ameeleza kuwa kinacholeta madhara katika moshi ni uwepo wa hewa ya cabon monoxide ambayo inakuwa na punji ndogo ndogo ambazo zikiingia kwenye damu inapunguza oxygen ambayo itasababisha mtu kuchoka, mwili kukosa nguvu na vifo vya ghafla hususan kama madirisha yamefungwa na mzunguko wa hewa sio mkubwa.
Dkt. Mahenge ameeleza kuwa moshi unaweza pia kusababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ya mapafu, saratani ya ngozi, magonjwa mbalimbali ya mfumo wa hewa na upumuaji kutokana na sumu iliyomo kwenye moshi.
Dkt. Mahenge ameeleza kuwa wao kama wataalamu wanapendekeza wananchi watumie nishati mbadala hususan gesi asilia badala ya kupikia kuni na mkaa wakati wote.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Waziri alipokelewa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Khalfan Haule katika Uwanja wa Ndege Musoma na baada ya hapo alitembelea ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kutia Saini kitabu cha wageni na kuwasalimia viongozi.
Aidha katika Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Makamba ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara na kupokea taarifa ya kitaalamu kuhusiana na madhara ya moshi kwa binadamu; ametembelea kikundi cha wanawake wanaokaanga dagaa katika eneo la Mwisenge na kufanya kikao na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) katika Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Mwembeni Complex.
Katika Wilaya ya Butiama Mheshimiwa Makamba amewasha Umeme nyumbani kwa mwananchi mmoja, amemtembelea Bibi Tereza Stephano ambaye amempatia jiko la gesi na kumhamasisha kutumia gesi, amezindua huduma ya Ni-Konect Mkoa wa Mara na kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Kisamwene.
Akiwa katika Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Makamba amezungumza na wananchi katika eneo la Nyamswa na kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Mara na mikoa ya jirani kwa njia ya matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa na kituo cha redio ya kijamii ya Bunda FM.
Kesho Mheshimiwa Makamba ataendelea na ziara yake katika Mkoa wa Simiyu na baada yah apo mikoa mingine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa