Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo amefanya ziara ya siku moja katika Mkoa wa Mara ambapo ametembelea Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) na kuelezea mpango wa Serikali kufanya maboresha makubwa katika hospitali hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na wagonjwa na waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mwalimu amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara imetenga zaidi ya shilingi bilioni 11 kwa ajili ya ukamilishaji wa Wing A ya hospitali hiyo kwa shilingi bilioni 7 na ufungaji wa miundombinu ya umeme kwa zaidi ya shilingi bilioni 4.
“Tayari mkandarasi wa kukamilisha Wing A ya jengo hilo ameshapatikana na mkandarasi wa kufunga miundombinu ya umeme ameshapatikana na wanatarajiwa kukamilisha kazi hizo mapema iwezekanavyo”, amesema Mhe. Mwalimu.
Aidha, Mhe. Mwalimu amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa fedha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la watoto wachanga wenye siku 0 hadi siku 28 katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Mhe. Mwalimu amesema jengo hilo litawahudumia watoto wenye uzito pungufu, watoto walio mahututi na wodi ya watoto wachanga wenye magonjwa yanayoambukiza ili kuweza kuwaokoa watoto wachanga wanaozaliwa ndani ya siku 28 za kwanza.
“Kwa sasa tumewaachia wataalamu wa Wizara ya Afya, mshauri mwelekezi wa mradi huo (Chuo Kikuu cha Ardhi) waangalie kama wodi hizo zinaweza kutokana na ukamilishaji wa jengo lililopo au tunahitaji kujenga jengo jingine maalum kwa ajili hiyo” amesema Mhe. Mwalimu.
Aidha, Mhe. Waziri ameeleza kuwa Serikali imetoa nafasi katika Hospitali Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa ajili ya Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) kuanzisha Kituo cha Mifupa ambacho kitahudumia wagonjwa kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.
Waziri wa Afya pia amesema Serikali imepanga kuitumia Hospitali hiyo kwa ajili ya tiba utalii na inalenga kuwavutia zaidi wagonjwa kutoka katika nchi za Kenya na Uganda ambazo zinapakana na Mkoa wa Mara na kutoka mataifa mengine duniani kuja kutibiwa hapo.
Akizungumza na wafanyakazi wa hospitali hiyo, Mhe. Mwalimu amewaahidi kupanga siku ya kuja kuzungumza nao na kuwataka kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa na kuwahudumia kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuridhia maombi ya Mkoa wa Mara ya kutoa eneo la ekari 20 katika hospitali hiyo kwa ajili ya ujenzi wa Skuli ya Afya ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia- Butiama.
“Chuo hiki kikiwa na wanachuo hapa tutapata baadhi ya wataalamu wa kusaidia katika utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara ikiwemo Hospitali hii” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuanzisha mchakato wa kupata umeme wa uhakika katika hospitali hiyo baada ya kutoa mkataba kwa mkandarasi Wakala wa Umeme wa (TEMESA) wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili yakutatua changamoto ya umeme katika hospitali hiyo.
Aidha, Mhe. Mtanda amemuomba Mhe. Waziri kuongeza watumishi zaidi wa sekta ya afya katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya hospitali hiyo na vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika Mkoa ili kuboresha huduma za afya.
Mhe. Mtanda amesema mbali na maboresho katika Hospitali ya Rufaa, kwa sasa OPD za Hospitali za Halmashauri zote zinafanyakazi na hospitali nyingine zinatoa huduma nyingi zaidi kulingana na hatua za ukamilishaji wa majengo na vifaa tiba.
Mkuu wa Mkoa pia amemhakikishia Mhe. Waziri kuwa ukarabati katika Hospitali ya Manispaa ya Musoma ambayo awali ilikuwa ni Hospitali ya Mkoa wa Mara unaendelea vizuri huku hospitali hiyo ikiwa inaendelea kutoa huduma kama ilivyokuwa awali.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Meya wa Manispaa ya Musoma, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Wataalamu kutoka Wizara ya Afya na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa