Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Mji wa Bunda katika uwanja wa stendi ya zamani na kuwahakikishia wananchi wa Kata ya Nyatwali kuwa malipo ya fidia yataanza kutolewa muda wowote kuanzia wiki ijayo.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa malipo yapo tayari na kuwataka wananchi kujiandaa kupokea fidia zao na kuhama katika eneo hilo kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Malipo ya fidia ya Nyatwali yameshatoka na mimi ninategemea muda wowote kuanzia wiki ijayo Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) litaanza kutoa fedha hiyo kwa wananchi wa eneo la Nyatwali” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kutenga maeneo maalum ambayo watauziwa wananchi watakaohama kutoka katika Kata ya Nyatwali kwa bei nafuu ili kuwasaidia watakaotaka kubaki ndani ya Wilaya ya Bunda kupata maeneo kwa haraka.
Mhe. Mtambi amewaelekeza Wakurugenzi hao kuitisha vikao maalum vya Mabaraza ya Madiwani kujadili suala la kutenga maeneo na kuwauzia wananchi hao wiki ijayo na kuagiza ofisi yake ipate taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo haraka iwezekanavyo.
Aidha, Mhe. Mtambi amewasistiza wananchi wa Nyatwali watakaolipwa fidia hizo kutumia fedha hizo kwa ajili ya kufanyia shughuli za maendeleo yao na familia zao.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara ameiagiza Halmashauri ya Mji wa Bunda kumkabidhi fidia ya viwanja viwili Bibi Monica Palapala, mkazi wa Bunda Stoo hadi kufikia Jumatatu tarehe 1 Julai, 2024 ili kufidia eneo lake lililochukuliwa na barabara baada ya kupima eneo hilo.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko ya Bibi Palapala ambaye alikuwa na shamba lake eneo la Bunda Stoo na baadhi ya eneo lake kupitiwa na barabara na kubakiwa na kiwanja kimoja badala ya viwanja vitatu alivyopimiwa awali.
aidha, Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuzingatia usafi kwenye makazi na biashara zao ili kuweza kuwavutia wawekezaji na watalii wanaoingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupumzika katika Mji wa Bunda.
Kanali Mtambi pia amewataka vijana kuunda vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vinaweza kusaidiwa mikopo au ujuzi na wataalamu wa Serikali na wadau wengine waliopo katika Mkoa wa Mara ili kuweza kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Bwana Peter Alphonce Chacha mkazi wa Mtaa wa Tamau, Kata ya Nyatwali ameipongeza Serikali kwa kulipa fidia wananchi wa eneo hilo, kwa sasa changamoto ni nyingi maana hawaruhusiwi kuliendeleza eneo hilo baada ya kufanyiwa tathmini.
Bwana Chacha amesema walikuwa wanaishi hapo kwa wasiwasi kwa kuwa walikuwa wanavamiwa na wanyama mara kwa mara kutoka SENAPA na japokuwa walikuwa wanalipwa fidia lakini ilikuwa haitoshi ikilinganishwa na mazao waliyokuwa wanapoteza.
Kwa upande wake, Bwana Ibrahim Gigita Joseph mkazi wa Mtaa wa Kariakoo, Kata ya Nyatwali amesema kwa muda wa miaka miwili tangu wafanyiwe tathmini kwa ajili ya kulipwa fidia walikuwa wanaishi kama kifungoni.
“Bora tulipwe tukaanzishe maisha mapya sehemu nyingine, tuwe huru na labda watoto wetu watakuja kupata kazi katika hifadhi hii hapo baadaye” amesema Bwana Joseph.
Mkutano huo umehudhuriwa na baadhi ya Maafisa kutoka Sektretarieti ya Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, Wenyeviti wa Halmashauri , Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri za Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa