Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene leo amefanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mara na kuzungumzia mpango wa Serikali kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ili kuibadilisha Manispaa ya Musoma.
Akiwahutubia wananchi wa Musoma, Mhe Simbachawene amesema katika mipango yake Serikali inampango wa kupanua treni ya kisasa ya SGR ifike Musoma, kujenga bandari kubwa na uwanja wa ndege wa kimataifa na miradi hii ikikamilika itaibadilisha kabisa Manispaa ya Musoma.
“Miradi hii haitafanywa kwa pamoja itafanywa kwa awamu ya miaka mitano mitano ili kuvutia watalii zaidi kuingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Mara kwa kuufugua mkoa huu katika sekta ya usafirishaji” amesema Mhe. Simbachawene.
Akizungumzia kuhusu treni ya SGR, Mhe. Simbachawene amesema mpango wa Serikali baada ya treni hiyo kufika Mwanza, kutakuwa na mradi mwingine wa kujenga treni hiyo kuja Musoma na itaunganishwa kuelekea Kenya, lengo likiwa ni kurahisisha usafirishaji wa mizigo ambayo itapunguza bei za bidhaa baada ya kufika Musoma.
Mhe. Simbachawene amesema Serikali pia inampango wa kupanua na kuimarisha Bandari ya Musoma ili kuvutia meli kubwa kuweza kuta nanga katika bandari hiyo na kuimarisha usafirishaji wa mizigo na abiria na uchumi wa Manispaa ya Musoma.
Mhe. Simbachawene amesema Serikali inampango wa kujenga uwanja wa ndege wa Kimataifa baada ya kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa uwanja uliopo ili kuwavutia watalii wengi zaidi kuingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kupitia uwanja huo wa Musoma.
Mhe. Simbachawene amesema kwa sasa Mkoa wa Mara umekuwa ukipokea watalii wengi wanaoingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti baada ya kutambua kuwa ni rahisi kuingia ukitokea Wilaya za Bunda na Serengeti.
Mhe. Simbachawene amesema ndani ya miaka mitatu Mkoa umepata fedha nyingi kutokana na ongezeko la watalii kuliko wakati mwingine wowote.
Wakati huo huo, Mhe. Simbachawene amewataka vijana kutokuyumbishwa na watu wasiopenda maendeleo na badala yake kuchukua fursa hiyo kufuatilia mambo yanayofanywa na Serikali na taasisi zake katika kuwaletea wananchi huduma mbalimbali za maendeleo.
Mhe. Simbachawene amesema kwa kasi ya maendeleo inayofanyika hapa nchini, amani na utulivu ukiendelea kwa miaka mingine 25, Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi, hivyo amewataka vijana kuilinda amani kwa nguvu zao zote.
Aidha, amewataka vijana kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Serikali Kuu wa mwaka 2025 ili kuwachagua viongozi bora wanaopenda maendeleo kuanzia kwenye mitaa, vijiji na vitongoji vyao hadi Taifa.
Ziara ya Mhe. Simbachawene inatarajiwa kuendelea kesho katika Wilaya za Rorya na Tarime na tarehe 3 Oktoba, 2024 katika Wilaya ya Serengeti na Butiama na kuhitimishwa tarehe 4 Oktoba, 2024 katika Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa