Serikali mkoani Mara inaendelea kufanya uchunguzi wa tukio la kupotea kwa Bwana Mango Kahuru (20) mkazi wa kijiji cha Kenyamosabi katika Wilaya ya Tarime wakati akichunga ng’ombe ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) tarehe 11 Desemba 2020.
Akizungumza na wananchi wa Kata za Kwishancha, Gorong’a na Nyanungu katika Shule ya Msingi Kinyamosabi leo tarehe 16 Desemba 2020, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amesema vyombo vya ulinzi na usalama vya Mkoa na Wilaya ya Tarime vinaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa bado uchunguzi unaendelea na tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime imetembelea eneo la tukio lililopo ndani ya hifadhi na kujionea hali halisi ya sehemu tukio lilipotokea” alisema Mheshimiwa Malima.
Mkuu wa Mkoa pia amewaomba wanafamilia na wananchi wa eneo hilo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola vinavyoendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ili uchunguzi uweze kukamilika kwa haraka na majibu yaweze kupatikana kutokana na tukio hilo.
Hata hivyo Mheshimiwa Malima amewaasa wananchi wa eneo hilo kuacha mara moja kupotosha ukweli juu ya tukio la kupotea kwa Bwana Kahuru kwani hamna mwenye uthibitisho wa taarifa mbalimbali za upotoshaji zinazosambazwa kuhusiana na tukio hilo.
“Tangu tukio hili limetokea kuna maneno mengi sana yametokea kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hili na ukiyaangalia maneno mengi ni ya uongo na uzushi, sasa ndugu zangu sheria zipo zinafanyakazi, tuache upotoshaji hausaidii wakati huu ambapo bado tunaendelea kumtafuta kijana wetu” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima amewaomba wananchi wa eneo hilo kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo wakati huu ambapo vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Aidha Mheshimiwa Malima amewaonya wananchi wa eneo hilo kuacha mara moja tabia ya kuanzisha migogoro isiyoisha katika eneo hilo ambapo tangu yeye awe Mkuu wa Mkoa huo miaka mitatu iliyopita ameshatatua migogoro mingi sana ikiwemo migogoro ya mipaka kati ya wananchi wa eneo hilo na SENAPA.
“Kwa Mkoa wa Mara, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inapakana na Wilaya za Serengeti, Butiama na Tarime, lakini pamoja na ukweli kuwa Tarime mnaeneo dogo zaidi la mpaka, lakini mmekuwa na migogoro mingi sana ukilinganisha na wilaya za Bunda na Serengeti ambazo mipaka yake ni mikubwa zaidi “ alisema Mhehsimiwa Malima.
Aidha Mheshimiwa Malima amewatahadharisha wananchi wa eneo hilo kuacha tabia ya kuingia hifadhini na kufunga waya za mitego na kuua wanyama pori ndani ya hifadhi pamoja na kufanya shuguli nyingine za kibinadamu.
“Hivi karibuni mmefunga mitego na mmeua zaidi ya wanyama 100 kwa wakati mmoja na mkawaacha hapo hapo wala hamkuchukua hizo nyama zote, huu ni uharibifu na ni kinyume cha sheria” alisema Mheshimiwa Malima.
“Kama kuna mtu yoyote anayewahamasisha kwenda kufanya uharibifu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti anawaongopea, serikali ipo kazini na taarifa zenu za kutega mitego kwa ajili ya wanyama tunazo na tunazifanyia kazi” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha aliwaagiza SENAPA kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ujirani mwema katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo ili kupunguza baadhi ya migogoro na wananchi hao kutokana na kukosa uelewa kuhusu sheria na namna wanavyonufaika na uwepo wa hifadhi hiyo.
Mheshimiwa Malima pia aliwataka viongozi wa vijiji hivyo kutoa taarifa za matukio mbalimbali yanapotokea kwenye vyombo la ulinzi na usalama, ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi yake ili malalamiko yao yaweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka zaidi na sio kusubiri viongozi wanapotembelea maeneo hayo.
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa ambaye aliambatana na Kamati za Ulinzi na Usalama, maafisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), SENAPA na watumishi wa serikali, alipokea maelezo na maoni ya familia, wananchi na viongozi waliokuwepo katika eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kenyamusabi Bwana Mwita Raphael Salima ameeleza kuwa katika miaka ya 2019 na 2020 watu watatu wanasadikiwa kuuawa na askari wa SENAPA na wengine kujeruhiwa baada ya kuingia katika hifadhi hiyo.
Aliwataja wanaosadikiwa kuuawa kuwa ni Matiko Kebohi Marwa, Mwita Mwita Sereka na Manga Kahuru Manga ambaye amepotea akiwa anachunga ng’ombe katika hifadhi hiyo na mpaka sasa hajulikani alipo.
“Aidha askari wamewajeruhi Marwa Masambe, Marwa Mwita Matutu na Bwana Marwa Chacha Wambura ambaye mpaka sasa amepata ulemavu wa kudumu” alisema Bwana Salima.
Aidha Bwana Salima aliomba SENAPA kuimarisha uhusiano na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kama ilivyokuwa hapo awali ili wananchi waweze kupata elimu ya uhifadhi na kusaidiaa katika kuilinda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa