Naibu Katibu Mkuu- Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula leo amefanya ziara katika Mkoa wa Mara na kutembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) Mkoa wa Mara kilichopo eneo la Mwisenge, Manispaa ya Musoma na kukitaka chuo hicho kuwa na ubunifu na kuongeza fani zinazofundishwa na Chuoni hapo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya Chuo hicho, Dkt. Rwezimula ameutaka uongozi wa Chuo kufundisha fani ambazo zinaweza kupata wanachuo wengi kutokana na mazingira ya Mkoa wa Mara na maeneo yanayokizunguka Chuo hicho.
“Huu ni Mkoa ambao kuna uchimbaji wa madini, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ziwa Victoria, nilitegemea Chuo hiki kitoe mafunzo kwenye fani za ufugaji wa samaki kwenye vizimba, masuala ya madini, utalii na zinazoendana na mazingira ya Mkoa wa Mara” amesema Dkt. Rwezimula.
Dkt. Rwezimula ameuagiza uongozi wa Chuo hicho kuongeza juhudi katika kujenga mahusiano na taasisi mbalimbali ili kuweza kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo kupata magari chakavu ambayo watayatengeneza na kuyatumia kwa ajili ya kufundishia.
Aidha, amekitaka Chuo hicho kuangalia uwezekano wa kumtafuta Afisa Uhusiano ili aweze kufanyakazi za kuunganisha Chuo na wadau mbalimbali watakaokisaidia Chuo katika kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Dkt. Rwezimula amekiagiza Chuo kufanya juhudi za maksudi za kuongeza idadi ya wanafunzi wakike na kutumia vizuri mafunzo kwa vitendo ya wanachuo wa chuo hicho katika kujenga mahusiano endelevu na waajiri wanaopokea wanafunzi hao.
Taarifa ya Chuo hicho imeonyesha kuwa chuo kilianzishwa mwaka 1986 na kilikuwa kinatumia majengo ya iliyokuwa Shule ya Msingi Mwisenge na kwa sasa Chuo kinafundisha mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika fani tisa na kina jumla ya wanafunzi 255.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo changamoto kinachoikabili chuo hicho ni pamoja na kukosekana kwa mabweni na kulazimu wanachuo wa mbali kuingia gharama kubwa za kupanga nyumba nje ya chuo hicho, kukosekana kwa uzio na upungufu wa magari, bajaji na pikipiki za kufundishia.
Changamoto nyingine ni uhaba wa nafasi za mafunzo kwa vitendo katika baadhi ya fani zinazotolewa chuoni hapo na kulazimisha chuo kuchukua wanachuo wachache ikilinganishwa na idadi ya waobaji katika fani hizo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uongozi wa VETA umeanza kuchukua hatua mbalimbali kuboresha chuo hicho na ikiwa ni pamoja na kujenga mabweni kwa siku za baadaye.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu katika Chuo cha VETA Mara ni mwendelezo wa ziara yake ambayo ilianza kwa kukagua Chuo cha VETA kinachoendelea kujengwa katika Wilaya ya Tarime, kusaini kitabu cha wageni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na baadaye kufunga mafunzo ya Walimu Wakuu wa Mkoa wa Simiyu katika Chuo cha Ualimu Bunda.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu aliambatana na Mdhibiti Ubora wa Kanda ya Ziwa Bi. Lucy Nyanda na Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga na viongozi wengine kutoka Wizarani.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa