Naibu Katibu Mkuu –Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula leo amefungua awamu ya kwanza ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi Walimu Wakuu wa Shule za Msingi za Mkoa wa Simiyu yanayofadhiliwa na Mradi wa BOOST na kusimamiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM).
Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo, Dkt. Rwezimula amewataka walimu hao kufuatilia kikamilifu mafunzo hayo na kwenda kubadilisha utendaji kazi katika vituo vyao vya kazi ili kuboresha elimu ya msingi hapa nchini.
“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatawawezesha kusimamia shule kwa ufanisi hasa wakati huu tunapoanza kutekeleza mitaala mipya iliyoanza kutumika mwaka huu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu” amesema Dkt. Rwezimula.
Dkt. Rwezimula amewataka Wakuu wa Shule kuongoza shule kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na kusimamia miradi ya elimu wanayotakiwa kusimamia kwa ufanisi.
Dkt. Rwezimula ameupongeza uongozi wa ADEM kwa kuendelea kutoa mafunzo ya uongozi kwa wasimamizi mbalimbali wa sekta ya Elimu hapa nchini ambayo yanaisaidia nchi katika kuboresha usimamizi wa sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo hayo Bwana Mashiku Thomas Ng’wandu ameeleza kuwa kwa awamu ya kwanza mafunzo hayo yamewahusisha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 285 kutoka Halmashauri za Bariadi, Itilima na Busega Mkoani Simiyu na yameanza tarehe 19-21 Februari, 2024.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo Walimu Wakuu katika uongozi, usimamizi na uendeshaji wa Shule za Msingi
Bwana Mashiku ameeleza kuwa awamu ya pili yatawahusisha Wakuu wa Shule 299 kutoka Halmashauri zilizobakia katika Mkoa wa Simiyu na yatafanyika Chuo cha Ualimu Bunda kuanzia tarehe 21-24 Februari, 2024.
Bwana Mashiku ameeleza kuwa katika mafunzo hayo, mahiri mbalimbali zinategemewa kuwezeshwa na wakufunzi kutoka ADEM wakishirikiana na baadhi ya wasimamizi wa elimu kutoka Mkoa wa Simiyu.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Emanuel Mollel ameeleza kuwa ADEM ina wataalamu wengi waliobobea katika mafunzo ya uongozi wa elimu na ameishukuru Wizara ya Elimu kwa akuendelea kuiamini na kuwapa kazi mbalimbali.
Dkt. Mollel ameeleza kuwa miungoni mwa kazi walizopewa na Wizara hiyo ni pamoja na mafunzo kwa Maafisa Elimu wa Mikoa ambayo yanatarajiwa kufanyika hivi karibuni katika Mji wa Bagamoyo.
Akizungumzia mafunzo yanayotolewa kupitia Mradi wa BOOST Dkt. Mollel ameeleza kuwa hadi sasa ADEM imeshatoa mafunzo kwa walimu zaidi ya 6700 katika awamu ya kwanza, na katika awamu hii wanategemea kutoa mafunzo kwa walimu zaidi ya 4000 katika mikoa mbalimbali.
Dkt. Mollel amewataka walimu kutumia mafunzo hayo katika kuboresha utendaji na usimamizi wa elimu ili kuonyesha manufaa ya mafunzo hayo.
Ufunguzi wa mafunzo hayo umehudhuriwa pia na Makaimu Katibu Tawala Wasaidizi Sehemu ya Mafunzo wa Mikoa ya Simiyu na Mara, Mwakilishi wa TAMISEMI, Mdhibiti Ubora wa Kanda ya Ziwa, Naibu Mtendaji Mkuu wa ADEM, wakufunzi wa mafunzo hayo na baadhi ya Wakuu wa Divisheni za Elimu kutoka Mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa