Wilaya ya Rorya imeomba upanuzi wa shughuli za mpaka wa Kirongwe uliopo katika Wilaya ya Rorya ili kuimarisha biashara za wananchi na kupunguza magendo katika mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo katika eneo hilo.
Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato wa Wilaya ya Rorya Bwana Samweli Chacha wakati akitoa taarifa katika kituo cha Kirongwe kilichopo katika Wilaya ya Rorya.
“Kwa sasa Rorya inawafanyabiashara wengi sana wanaofanya biashara zao kati ya miji iliyopo mpakani na Mji wa Shirati lakini kituo hiki cha Kirongwe hakiruhusu kupitisha mizigo, mizigo inatakiwa kupitishiwa katika mpaka wa Sirari tu” alisema Bwana Chacha.
Bwana Chacha ameeleza kuwa kwa upande wa Kenya, tayari wamejenga kituo kikubwa chenye wataalamu wote wanaohitajika na wapo tayari kwa ajili ya kupitisha biashara eneo hilo lakini kwa upande wa Tanzania kituo hicho kipo tu kwa ajili ya kuzuia magendo na kupitisha watu.
Meneja huyo ameeleza kuwa kituo hicho kikianza kupitisha biashara kitaimarisha biashara za wananchi wa Rorya na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Bwana Chacha ameeleza kuwa kwa sasa Serikali ya Tanzania tayari imeandaa eneo la kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika eneo hilo hata hivyo taratibu za kubadilisha kituo hicho bado hazijakamilika.
Kwa upande wake Mdhibiti wa Magendo katika Mkoa wa Mara Bwana Robert Insumagi ameeleza kuwa kutokana na umbali kupitisha biashara zao katika mpaka wa Sirari wananchi wenngi wa eneo hilo wanapitisha biashara zao kimagendo jambo ambalo sio sawa.
“Wananchi wanalazimika kwenda kupitisha kihalali mpaka wa Sirari ambao upo umbali wa zaidi ya kilomita 70 kutoka eneo hilo” alisema Bwana Insumagi.
Bwana Insumagi ameeleza kuwa magendo makubwa wanayopambana nayo ni ya bidhaa ambazo Kenya bei ni nafuu ikilinganishwa na Tanzania kama vile sukari, mafuta ya kupikia na sementi.
Ameeleza kuwa katika Wilaya ya Rorya kuna vipenyo vilivyo rasmi viwili na visivyo rasmi 11 ambavyo wananchi wanavitumia kupita kwenda katika maeneo ya jirani upande wa Kenya na mara nyingi hupitisha magendo yao kutumia vipenyo hivyo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alitembeleza vituo vya mpakani vya Kirongwe, Kogaja na Ikoma katika Wilaya ya Rorya na mpaka wa Sirari katika Wilaya ya Tarime.
Akizungumza katika kuhitimisha ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amewataka watendaji wote wanaohusika na ulinzi na ukaguzi wa mipaka kufanyakazi kwa weredi.
“Sisi kama serikali tunawategemea ninyi kwa sehemu kubwa katika kuendesha shughuli zake hapa mpakani, kwa hiyo tunahitaji ushirikiano kati yenu, weredi na ubunifu katika kutekeleza majukumu yenu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Bwana Apoo Tindwa kufanyiakazi suala ya maegesho ya malori na upatikanaji wa maji ya uhakika katika eneo la Sirari.
Aidha ameahidi kufuatilia changamoto mbalimbali alizozipokea kutoka kwa maafisa wa mipaka hiyo kwa mamlaka zinazohusika ili kuimarisha ulinzi wa mpaka na biashara kati ya Kenya na Tanzania.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa