Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara leo imepitisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya Mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yenye jumla ya shilingi 356,879,507,000 kwa ajili ya mishahara miradi ya maendeleo na matumizi menginey.
Akiwasilisha mpango na Bajeti katika kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mpango na Uratibu Bwana Emmanuel Mazengo amesema kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 13 ukilinganisha na kiasi cha shilingi 317,045,656,000 kilichoidhinishwa mwaka wa fedha 2023/2024.
“Fedha zinazoombwa zinajumuisha shilingi 263.053,556,000 za matumizi ya kawaida na shilingi 93,825,951,000 za shughuli za maendeleo” amesema Bwana Mazengo.
Bwana Mazengo ameeleza kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 10,328,357,000 ni kwa ajili ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara wakati shilingi 346,551,043,000 ni bajeti ya jumla ya Halmashauri tisa za Mkoa wa Mara.
Bwana Mazengo amevitaja vipaumbele vya bajeti katika mwaka wa fedha 2024/2025 ni pamoja na kuendelea na uboreshaji wa sekta ya elimu; kuendelea na uboreshaji wa sekta ya afya; huduma za utawala na uchumi na uzalishaji mali.
Kikao hicho pia kimepokea na kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya maendeleo ya sekta ya maji; mapendekezo na mpango wa bajeti ya sekta ya nishati (TANESCO); taarifa kuhusu mitambo ya uchimbaji wa visima vya maji na uchorongaji madini iliyopokelewa katika Mkoa wa Mara.
Mambo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na maombi ya vijana wanaoshiriki mradi wa BBT kupatiwa eneo la kilimo na maombi ya kuigawanya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ili kuwasaidia wananchi kupata huduma kiurahisi.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda kimeridhia masuala yote isipokuwa suala la mgawanyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambalo kikao kimeliacha kwa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kulifanyiakazi suala hilo.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na viongozi wa vyama vya siasa, wabunge wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Meya na wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, viongozi wa dini na waalikwa wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa