RC SIMIYU MGENI RASMI NANENANE KANDA YA ZIWA MASHARIKI
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mheshimiwa Dokta Yahya Nawanda kesho anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima (NANENANE) Kanda ya Ziwa Mashariki katika viwanja vya Nyakabidi, Bariadi Mkoa wa Simiyu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo, shughuli katika uwanja wa maonyesho zitaanza saa mbili kamili asubuhi kwa wageni waalikwa kuanza kuwasili katika viwanja vya Nyakabindi.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Mheshimiwa Nawanda akiambatana na wakuu wa mikoa wa Kanda ya Ziwa Mashariki na viongozi wengine, atatembelea mabanda ya maonyesho kuanzia saa 6.20 na baadaye kuwahutubia wananchi wa Kanda ya Ziwa Mashariki katika viwanja vya Nyakabindi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee kesho atakagua mabanda ya Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kabla ya Mgeni Rasmi kupita katika mabanda hayo.
Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Mzee atakagua mabanda hayo kuanzia saa tatu na nusu asubuhi akiambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo amekagua mabanda ya maonyesho ya Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Akiwa katika mabanda hayo, Katibu Tawala aliambatana na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara pamoja na viongozi wa Halmashari za Mkoa wa Mara.
Mikoa mitatu inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki ni Mara, Shinyanga na Simiyu ambao ndio mwenyeji wa maadhimisho hayo yanayofanyika katika eneo la Nyakabidi, wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa