Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amekutana na kufanya mazungumzo na wazee wa Manispaa ya Musoma katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtanda amewaomba wazee kumpa ushirikiano yeye na viongozi wengine wa Serikali katika kuuongoza Mkoa wa Mara na hususani kwa kutoa maoni, ushauri na mawazo ya namna ya kuujenga Mkoa wa Mara.
“Ninawaomba sana mtupatie ushirikiano katika kutekeleza yale yote tunayotakiwa kuyafanya katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mtanda.
Mhe. Mtanda amewaahidi wazee kuwa Ofisi yake itasimamia upatikanaji wa huduma stahiki za wazee na kusimamia udhibiti masuala ya ukatili dhidi ya wazee na watu wengine.
Mheshimiwa Mtanda ameeleza kuwa lengo la kukutana nao ni kujitambulisha kwao ili wampe Baraka zao kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuwasilisha kero zao, ushauri na maoni ofisini kwake na ofisi za viongozi wa Serikali ili waweze kuzifanyia kazi.
Wakati huo huo, Mhe. Mtanda ameziagiza Halmashauri za Mkoa wa Mara kuwafanyia sensa wazee na kutoa vitambulisho vya wazee wanaostahili ili waweze kupata huduma za matibabu bure kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Aidha, amezitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa mabaraza ya wazee yanafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na serikali kuhusu mabaraza ya wazee.
Mheshimiwa Mtanda pia ameongelea wajibu wa jamii na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya vijiji, mitaa, Kata, Halmashauri na Mkoa katika kuwatunza wazee wanaoishi katika maeneo yao.
kwa upande wao, wazee wa Manispaa ya Musoma wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukutana nao na kumuahidi kumpatia ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akizungumza katika kikao hicho Bibi Amina Magoti ambaye ni Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Mara amesema kikao hicho kimekuja wakati muafaka wakati Mkoa unajiandaa kufanya maadhimisho ya kupinga Ukatili dhidi ya Wazee.
Aidha, Bibi Amina ameeleza kuwa Mkoa wa Mara una rasilimali nyingi na eneo kubwa la kilimo na kumuomba Mkuu wa Mkoa kutembelea maeneo hayo.
Aidha, wazee hao wamemuomba Mkuu wa Mkoa na serikali kwa ujumla kufufua viwanda na kujenga viwanda vipya ili watoto wapate ajira.
Wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Magiri Benedicto Malegesi , Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Msalika Robert Makungu, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na lishe Dkt. Zabron Masatu, Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. Wiliam Gumbo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bwana Bosco Ndunguru.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa