Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 30 Oktoba, 2023 amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo ametoa muda wa kukamilisha miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Mhe. Mtanda amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mtana kinachojengwa na fedha za Serikali Kuu shilingi milioni 550 na Halmashauri shilingi milioni 250 ambapo ujenzi wake unaendelea na baadhi ya majengo yameanza kutoa huduma na kumtaka mkurugenzi kukamilisha mradi huu ndani ya mwezi mmoja.
“Mganga Mkuu wa Halmashauri na Mhandisi hakikisheni mradi huu ndani ya mwezi mmoja unakamilika na Mhe. Diwani ninaomba unipigie picha na kunitumia kama mradi utakuwa umekamilika” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda amekemea kitendo cha Halmashauri hiyo kuongeza shilingi milioni 250 katika mradi huo ambao sehemu nyingine unatumia shilingi milioni 500 tu hadi kukamilika.
Aidha, Mhe. Mtanda ametembelea Shule ya Sekondari Mtana ambayo inajengwa kupitia mradi wa maendeleo ya elimu ya Sekondari (SEQUIP) katika Kijiji cha Mtana na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kukamilisha mradi huo ndani ya siku 14.
Aidha, amekemea kitendo cha Halmashauri hiyo kukaa na fedha muda mrefu kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo jambo ambalo amesema halikubaliki katika Mkoa wa Mara.
Katika ziara hiyo pia ametembelea mradi wa maji eneo la Nyarero na kumtaka Meneja wa RUWASA na Meneja wa TANESCO Wilaya ya Tarime kufunga umeme na kuhakikisha maji yanatoka ndani ya siku 10 ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Katika kuhitimisha, Mhe. Mtanda alifanya mkutano na wananchi wa kitongoji cha Nyamichere, Kijiji cha Nyikunguru na kuwaasa wananchi kuacha kuvamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na badala yake kutafuta shughuli nyingine za maendeleo.
Aidha, Mheshimiwa Mtanda alisikiliza kero na maoni ya wananchi na kuahidi kulitafutia ufumbuzi suala la barabara inayoingia katika kijiji hicho ambayo wananchi wamesema ilifungwa na mgodi wa North Mara.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, watendaji wa Halmashauri na taasisi nyingine za umma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa