Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) leo imetembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya kujitambulisha na kusaini kitabu cha wageni na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda katika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza baada ya kupokelewa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Mabula ameupongeza Mkoa wa Mara kwa mapokezi mazuri tangu Kamati hiyo ilipowasili tarehe 20 Machi, 2024 katika Wilaya ya Tarime mpaka sasa.
“Kwa niaba ya Kamati, ninaomba kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo tuliyoitembelea na kukagua, miradi yote imesimamiwa vizuri, hongereni sana” amesema Mhe. Mabula.
Aidha, Mhe. Mabula amemshukuru Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. William Gumbo kwa mapokezi mazuri katika Manispaa ya Musoma tangu Kamati hiyo ilipowasili jana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda ameikaribisha Kamati ya LAAC na kuihakikishia kuwa miradi yote inayotekelezwa katika Mkoa wa Mara ipo katika viwango vya ubora vinavyotakiwa na Mkoa umekua ukiwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Kwa Mkoa wa Mara hatucheki na wahalifu na tumekua tukichukua hatua kwa wale wote waliotumia fedha za umma kinyume na utaratibu na tuna kesi mbalimbali zilizofunguliwa kwa watu wanaotuhumiwa kufuja fedha za umma” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ametoa mfano wa watumishi na wananchi walioiba mifuko 1,200 ya cementi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara ambao kwa sasa wameshafikishwa mahakamani.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Mhe. Mtanda ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa wa Mara unachangia pato la taifa kwa shilingi bilioni 130-140 kwa mwaka kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini katika mgodi mkubwa mmoja na migodi ya kati minne na wachimbaji wadogo zaidi ya elfu kumi waliopo katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda ameyataja mapato mengine kutoka Mkoa wa Mara yanatokana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo ni asilimia 36 ya eneo lote la Mkoa wa Mara, ambayo kwa mwaka huliingizia taifa mapato ya shilingi bilioni 138 kupitia utalii wa wageni kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania.
Aidha, Mhe. Mtanda amesema Mkoa pia umezungukwa na Ziwa Victoria ambapo asilimia 36 za eneo la Mkoa wa Mara ni Ziwa Victoria na Wilaya nne kati ya Wilaya sita za Mkoa wa Mara zinapakana na Ziwa Victoria na hivyo kuufanya uchumi wa Mkoa na hususan wananchi wake kutegemea pia shughuli za uvuvi katika mito na Ziwa Victoria.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa mbali na shughuli hizo, wananchi wa Mkoa wa Mara pia ni wafugaji na wakulima wazuri na hivyo uchumi wa wananchi wengi hutegemea shughuli za kilimo na ufugaji.
Mapokezi hayo yamehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Meya wa Manispaa ya Musoma, Maafisa kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa