Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ameendelea na ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo ametembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kuagiza kupatiwa taarifa ya ukaguzi iliyofanywa na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuhusu matumizi ya fedha katika ujenzi wa hospitali hiyo.
Akizungumza katika hospitali hiyo Mhe. Mtanda ameahidi kuwachukulia hatua watumishi wote watakaotajwa kukiuka taratibu, uzembe au kuiba fedha katika ujenzi wa hospitali hiyo.
“Watu wote waliohusika kwa namna mmoja au nyingine nitahakikisha wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria haraka iwezekanavyo” amesema Mhe. Mtanda na kumtaka Mkurugenzi kukamilisha kwa haraka majengo yanayoendelea kujengwa ili kupanua huduma katika hospitali hiyo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na uongozi wa Kata ya Nyamswa kukamilisha ulipaji wa fidia kwa Bibi Mary Wambura (71) anayedai fidia ya shilingi milioni 22 ili kuhama katika nyumba yake iliyopo ndani ya eneo la hospitali hiyo.
Tayari, Kata ya Nyamswa imemjengea nyumba mbadala ya kuhamia katika eneo jingine lakini makubaliano yalikuwa alipwe pia fidia hiyo kwa ajili ya mashamba yake ili ahame kupisha mradi wa hospitali hiyo makubaliano ambayo hayajakamilishwa tangu mwaka 2009.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amewataka wananchi wa eneo la Mariwanda kuwa makini wakati wa kuchagua kaya zitakazonufaika na Mpango wa Kaya Maskini (TASAF) ili wanufaika wote wa mfuko huo wawe na sifa za kuwezesha kunufaika na TASAF.
Aidha, amewataka Watendaji wa Vijiji, Kata na mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuhakikisha kuwa watu wote wanaostahili kuwemo kwenye mpango huo wanakuwemo na wasiostahili wanaondolewa.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amezungumza na wananchi katika eneo la Mariwanda na kukagua mradi wa maji eneo la Mariwanda, miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Shule za Sekondari za Mariwanda na Tirina katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya na wawakilishi wa Makatibu Tawala wasaidizi sehemu za Elimu na Miundombinu, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi wa Halmashauri, baadhi ya watumishi wa Halmashauri na taasisi zilizopo katika Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa