Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ameanza ziara katika Mkoa wa Mara kukagua miradi inayotekelezwa katika sekta za Elimu na Afya na kuwataka wafanyakazi na wananchi kufanyakazi kwa bidii.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo katika miradi mbalimbali aliyoitembelea katika Manispaa ya Musoma ambapo amesema bila kujituma katika kufanya kazi kwa bidii hamna mafanikio.
“Vitabu vyote vya dini vinahimiza watu kujituma katika kufanyakazi, rai yangu tufanyekazi kwa bidii na maarifa ili hata ukikosa mafanikio, juhudi yako katika kazi itaonekana” amesema Mhe. Mtanda.
Mheshimiwa Mtanda amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kukamilisha ujenzi wa miradi ya elimu kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma katika miradi hiyo.
Aidha, baada ya kupewa taarifa za changamoto mbalimbali zinazoikabili Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mhe. Mtanda ameahidi kufuatilia suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika na ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali hiyo Wizara ya Afya.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ametembelea mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu (two in one) katika Shule ya Sekondari Kigera Mwinyale, ujenzi wa vyumba vya madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma, ujenzi wa shule mpya katika eneo la Bweri Bukoba.
Aidha, katika ziara hiyo amekagua, kupanda miti na kuzungumza na wafanyakazi na wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa).
Kesho Mkuu wa Mkoa ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Bunda ambapo atatembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara, Shule ya Sekondari ya Kasuguti, Shule ya Sekondari ya Mariwanda na Shule ya Sekondari ya Bunda Mjini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa