Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuzungumzia mpango wake wa kuanza kusikiliza kero za wananchi kila siku ya jumanne kuanzia tarehe 01 Juni, 2024.
Akizungumza na watumishi hao, Mhe. Mtambi amesema atafungua kliniki maalum ya kusikiliza kero za wananchi akishirikiana na wataalamu mbalimbali waliopo katika Mkoa wa Mara.
“Huu utakuwa ni utaratibu wa kudumu kwa kila siku ya Jumanne tutasikiliza kero za wananchi ambapo wataalamu watazichakata na kila siku ya Ijumaa tutatoa mrejesho au maamuzi ya kero za wananchi waliosikilizwa wiki hiyo baada ya mimi kujiridhisha na mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema atahakikisha kero zote zitakazoletwa na wananchi zinasikilizwa na viongozi na watendaji wa umma katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa amani.
“Tufungue milango ya ofisi za Serikali, tuwasikilize na kutatua changamoto za wananchi na kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, sheria na taratibu za utumishi wa umma” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi pia amewataka Wakuu wa Wilaya, wakuu wa taasisi za umma, wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Mara kutenga siku ya kusikiliza kero za wananchi na kutatua migogoro yao kwa kuzingatia sheria, busara na maoni ya wananchi wa eneo husika.
Mhe. Mtambi amewataka watumishi wa Serikali kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa wao ni wawakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye maeneo wanayotolea huduma na kuongeza kuwa watumishi wanauwezo wa kuwafanya wananchi waipende Serikali yao au waichukie.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amesikiliza kero za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kufuatilia kwa ukaribu suala la kumpandisha cheo Bwana Lameck Chegeni, Mtendaji wa Kijiji cha Kano katika Kata ya Natta.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Serengeti kumpatia ajira ya muda Mtaalamu wa TEHAMA Bwana Mathias Ngola Samwel ambaye anajitolea katika Halmashauri hiyo kuanzia mwaka 2021.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa